Thursday, December 5, 2019

MREJEO (UP DATE) WA TAARIFA YA VIMBUNGA PACHA KATIKA BAHARI YA HINDI.


Dar es Salaam, 05 Disemba 2019:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa mrejeo wa taarifa iliyotolewa tarehe 04 Disemba 2019 kuhusu uwezekano wa kutokea vimbunga pacha katika Bahari ya Hindi kutokana na kuwepo kwa migandamizo midogo ya hewa.

Mgandamizo mdogo wa hewa uliopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (karibu na kisiwa cha Madagascar) umeendelea kuimarika na kuelekea kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar na unatarajiwa kuendelea kusababisha vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo machache ya Pwani ya Kaskazini ya nchi yetu kati ya leo terehe 5 na 6 Disemba 2019. 

Tahadhari ya vipindi vifupi vya mvua kubwa kwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es salaam na Pwani na angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe inaendelea.

Kwa upande mwingine, mgandamizo mdogo wa hewa katika pwani ya Somalia umeimarika na kufikia kiwango cha kimbunga kijulikanacho kwa jina ‘Pawan’. Kimbunga ‘Pawan’ kinatarajiwa kuingia katika pwani ya Somalia, hivyo hakitarajiwi kuwa na madhara katika nchi yetu.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hiyo katika bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...