Tuesday, April 30, 2024

​TMA YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA UBORA NA USAHIHI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA
















Morogoro; Tarehe 30 Aprili 2024;


Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wamekutana kupitia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF, Morogoro Tarehe 30 Aprili 2024, kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia maazimio ya Baraza lililopita pamoja na kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025. Baraza hilo lilifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari.

 

Mhe. Jaji Mshibe aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa wakati, taarifa ambazo zimesaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kuchukua hatua stahiki. Pongezi hizo zilitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Emmanuel Mpeta, viongozi wa TUGHE Taifa, Wizara na TMA.

 

“Kwa namna ya pekee niendelee kuwapongeza Menejimenti na wafanyakazi wote wa TMA kwa kuendelea kutoa na kusambaza kwa wakati utabiri bora ambao unasaidia kuokoa Maisha ya watu na mali zao, ambapo kwa mvua za vuli zilizoambatana na EL NINO kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa asilimia 98”. Alisema Mhe. Jaji Mshibe.

 

“Aidha, naendelea kuwakumbusha utendaji kazi wenye weledi na unaozingatia sheria na taratibu za kazi, sisi sote tukashirikiane kutimiza majukumu yetu ili kwenda sambamba na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee”.” Alisisitiza Jaji Mshibe.

 

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa lengo la kikao hicho cha Baraza ni kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka katika mwaka wa fedha 2023/2024.

 

Aidha, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imeainisha kazi zilizotekelezwa katika kipindi tajwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mikakati  ya kutatua changamoto husika.

 

“Mafanikio yaliyopatikana yamechagizwa na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania katika kuijengea Mamlaka uwezo wa kitaasisi, ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kununua vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, pamoja na uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma.” Alizungumza Dkt. Chang’a. 

 

Baraza hili limejumuisha wajumbe kutoka vituo vyote vya TMA Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa falsafa ya “Kwa maendeleo endelevu ya TMA, Tushirikishane, Tuimarishane na Tutegemezane” na pia ni utekelezaji wa Dira ya TMA “Kuwa kitovu bora cha huduma za hali ya hewa zinazowasaidia WADAU wote kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”.

Friday, April 19, 2024

TANZANIA YACHAGULIWA MAKAMU WA RAIS WA TUME YA SHIRIKIA LA HALI YA HEWA DUNIANI

Mhe. Balozi wa Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva, Dkt. Abdallah Posi (aliyekaa upande wa kulia) akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu na Huduma za Ufundi - TMA, Dkt. Pascal Waniha baada ya kutangazwa kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya INFCOM kupitia Mkutano wa Tume hiyo uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.
Dkt. Pascal Waniha (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wapya wa Tume ya INFCOM mara tu baada ya kuchaguliwa katika nafazi zao kupitia Mkutano wa Tume hiyo uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Washiriki wa Mkutano wakisikiliza matokeo ya uchaguzi wa viongozi wapya waliochaguliwa kupitia Mkutano wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Washiriki wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya INFCOM wakiwa katika picha ya pamoja kupitia Mkutano wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Geneva, Uswisi: Tarehe 18/04/2024

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) inayosimamia uangazi, miundombinu na mifumo ya taarifa za hali ya hewa (WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems - INFCOM). Katika uchaguzi huo Tanzania iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi, TMA, , Dkt. Pascal Waniha. 

Dkt. Waniha amechaguliwa katika nafasi hiyo  tarehe 18 Aprili, 2024 katika uchaguzi wa viongozi wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Mkutano wa tatu wa Tume hiyo (Third Session of the WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems- INFCOM-3)”, unaoendelea katika makao makuu ya WMO, Geneva- Uswisi tarehe 15 hadi 19 Aprili, 2024.

Uchaguzi wa Tume ya INFCOM umefanyika kufuatia muda wa viongozi waliokuwa madarakani kumaliza muda wao ambapo viongozi hao walichanguliwa mwaka 2021 na  waliongoza Tume ya INFCOM katika kipindi cha miaka minne (2020/21 – 2023/24). Uongozi wa juu wa Tume ya INFCOM unaundwa na Rais wa Tume akisaidiana na Makamu watatu wa Rais. Wagombea katika nafasi ya Makamu wa Rais walikuwa wanne (4), kutoka Tanzania, Czech, Hong Kong-China na India. Katika kinyang’anyiro hicho zilihitajika nafasi tatu na viongozi wapya waliochaguliwa ni Rais wa Tume hiyo, Bw. Michel Jean (Canada) ambaye anaendelea katika nafasi yake, na Makamu wa Rais  ambao ni  Dkt. Pascal Waniha (Tanzania), Dk. Chan Pak Wai (Hong Kong, China) na Dkt. Jan Danhelka (Jamhuri ya Czech).

Tume ya INFCOM ni mojawapo ya mihimili mikuu mitatu inayounda Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). Mihimili hiyo ni: (1) Tume inayosimamia uangazi, miundombinu ya hali ya hewa na mifumo ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Observation, Infrastructure and Systems - INFCOM); (2) Tume inayosimamia Matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Weather, Climate, Hydrological, Marine and Related Environmental Services and Applications - SERCOM) na Bodi ya Utafiti (Research Board). Dkt. Waniha atakuwa miongoni mwa viongozi wapya wa Tume ya INFCOM watakaoiongoza Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne (2024- 2028).

Dkt. Waniha ni Mtaalamu mbobezi wa hali ya hewa katika eneo la utabiri wa hali ya hewa kwa kutumia modeli (Climate Modelling and Numerical Weather Prediction -NWP) kwa takribani miaka 29, ambapo ametoa mchango mkubwa katika fani ya hali ya hewa ndani na nje ya Tanzania hususan katika WMO kupitia vikosikazi mbalimbali vya kuboresha miundombinu na huduma za hali ya hewa. Kuchaguliwa kwake katika nafasi hii ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ikizingatiwa kuwa nchi nyingi za Afrika zina changamoto ya upungufu wa miundombinu na teknolojia ya miundombinu ya hali ya hewa. Miundombinu ya hali ya hewa ni muhimu katika kupima na kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. 


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...