Friday, June 3, 2022

TAARIFA POTOFU INAYOSAMBAA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU HALI YA BARIDI HAPA NCHINI


 

Dar es Salaam, Tarehe 03 Juni 2022:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa potofu kuhusu hali ya baridi inayoendelea nchini. Taarifa hiyo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza, “kuanzia kesho hadi Agosti 22 mwaka huu kutakuwa na baridi zaidi kuliko miaka ya nyuma”. Taarifa hiyo potofu imehusisha Aphelion. Tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa dunia kwenye mfumo wa jua (solar system). Hata hivyo, mchango wake katika mwenendo wa hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine ni mdogo katika maeneo yetu kutokana na kuwa karibu na Ikweta.

Kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti kila mwaka, ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi hapa nchini ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali. Utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa na TMA tarehe 1 Juni 2022 unaonesha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Viwango vya joto la chini vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 140C hadi 260C kwa maeneo ya ukanda wa pwani, kati ya nyuzi joto 40C hadi 140C kwa maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi na kati ya nyuzi joto kati ya 100C hadi 200C kwa maeneo mengine ya nchi. Aidha, TMA imetoa tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa. Tahadhari hiyo ni kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Alhamisi tarehe 2 na inatarajiwa kudumu hadi tarehe 6 Juni 2022 na ambayo itakuwa ikihuishwa kila inapobidi.

TMA inapenda kuwakumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, TMA ndio taasisi pekee yenye jukumu la kutoa taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa Umma na kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa kutoka katika vyanzo visivyo rasmi kwa mujibu wa kifungu cha 27 na 31(5) cha Sheria hiyo.

Wednesday, June 1, 2022

KIPUPWE 2022: SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUCHUKUA TAHADHARI YA VIPINDI VYA BARIDI NA UPEPO MKALI VINAVYOWEZA KUJITOKEZA.


 

Dar es Salaam, Tarehe 01/06/2022

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2022. Taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, alisisitiza sekta mbalimbali kuchukua tahadhari za vipindi vya baridi na upepo mkali vinavyoweza kujitokeza nchini.

“Katika kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi ya nchi, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa mwezi Juni na Julai huku vipindi vya baridi kali vikitarajiwa katika maeneo yenye miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi, hivyo ni vyema sekta mbalimbali kuchukua tahadhari ya athari zinazoweza kujitokeza”. Alisisitiza Dkt. Chang’a

Dkt. Chang’a aliongezea kuwa hali ya joto la bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la bahari, kusini-mashariki mwa bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) hali inayotarajiwa kusababisha ukavu katika msimu huo, japo upepo unaotarajiwa kuvuma kutoka kusini mashariki na mashariki unaweza kuleta unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani).

Aidha, jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kuzingatia tahadhari za upepo mkali zitakazotolewa na TMA pale zitakapojitokeza.

Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...