Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Uwekezaji) Dorothy Mwaluko amelielekeza Jukwaa la Taifa la
Usimamizi wa Maafa nchini kutoa ushauri wa kitaalamu unaojikita katika hatua ya
kabla ya maafa kutokea na sio kujikita wakati wa maafa yanapotokea kama
ilivyozoeleka, kwa kuwa ushauri wa namna ya kuzuia na kujiandaa na maafa kabla
ya maafa kutokea huweza kupunguza
madhara ya maafa na rasilimali zinazohitajika katika upunguzaji wa madhara
hayo.
Ameyasema hayo leo Jijini Dodoma
tarehe 16 Desemba, 2019, wakati akifungua kikao cha Jukwaa hilo ambapo
amebainisha kuwa wakati wa kukabili majanga na maafa kunakuwepo na mipango
mingi ambayo hutekelezwa na wadau wa Usimamizi wa maafa na kwa uchache wakati
wa urejeshaji hali wa maafa, lakini
mipango ya kujiandaa na kuzuia maafa
ambayo hufanyika kabla ya maafa kutokea
kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara ya maafa yatakapotokea huwa haitekelezwi.
“Tumekuwa na maafa hapa nchini
ambayo yameleta madhara nchini,
itakumbukwa ajali ya moto mjini Morogoro hivi karibuni, tujiulize kuna
mipango inayoendelea katika kuzuia majanga hayo, yapo maafa ya mvua yanaendelea
kutokea, lakini je ipo mipango ya kabla
ya maafa kutokea, lakini pindi maafa yakitokea wadau wa usimamizi wa
maafa hujitokeza na kuanza kukabili maafa, sasa nataka nguvu nyingi ielekezeni
kwenye mipango ya kabla ya maafa kutokea na hata ikibidi ainisheni majanga
yanayoweza kutokea kwenye maeneo husika ili jamii iweze kujiandaa na kuyazuia
maafa husika kabla yakutokea“ Amesisitiza Mwaluko.
Aidha, amelielekeza Jukwaa hilo
kuupitia Mkakati wa Taifa wa Kupunguza athari za maafa na kuhakikisha kuwa
unaendana na uhalisia wa hali ya majanga yanayotokea katika jamii ili uweze
kutekelezeka kwa kuweka malengo yenye uhalisia, huku akisisitiza kuwa ni vyema
mkakati huo ukatafsiriwa kwa Kiswahili ili uweze kutumiwa vyema na walengwa
kuanzia ngazi ya msingi ya maafa ambayo ni kamati za vijiji.
Katika hatua nyingine Katibu
Mkuu, Mwaluko amelielekeza Jukwaa hilo
kuwa na ushirikiano miongoni mwa wadau wa jukwaa hilo kwa kila mdau kuainisha
majukumu yake na namna anavyoyatekeleza majukumu yake, ili kuweza kujua jukumu
la kila mdau na anafanya nini na kwa
wakati gani na hatimaye mipango ya kuimarisha Usimamizi wa maafa iwe
inayotekelezeka.
“Kupunguza madhara ya maafa ni suala
mtambuka lenye mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo.Wakati mwingine
wananchi wamekuwa wakipata madhara kwa kukosa uelewa hivyo ni vyema kila mdau
kuwajibika katika majukumu yake kwa kutoa fursa ya uratibu wa usimamizi wa
maafa kwa ushirikiano wa wataalamu
wa fani mbalimbali” Amesema,
Mwaluko
Awali akiongea katika kikao hicho,
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa , Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy
Matamwe, ameeleza kuwa Jukwaa hilo ni chombo cha kisheria ambacho kipo kwa
ajili ya kutathmini na kutoa ushauri wa kitaalam kwa serikali kuhusu majanga ya
aina zote, ambapo Jukwa hilo linaundwa
kwa kuzingatia Kifungu cha 40 cha Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.7 ya mwaka
2015.
Kikao hicho
kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania kupitia ufadhili wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kidunia ya
Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa ya GFCS (Global
Framework for Climate Services Adaptation Programme in Africa (APA)
II).
Jukwaa hilo ambalo linajumuisha
wataalamu wa fani mbali mbalimbali kwa kujumuisha sekta ya umma na sekta
binafsi, mashirika ya kimataifa na umoja wa mataifa na asasi za kiraia jukumu
lake la msingi ni kutoa ushauri maeneo ya kipaumbele katika usimamizi wa
maafa kwa uratibu na ushirikishawaji wa wadau ili kufanikisha kujumuisha
upunguzaji wa madhara ya maafa katika mipango na sera za maendeleo ya taifa na
katika misaada ya kibinadamu.
CHANZO: OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment