Wednesday, October 23, 2019

TMA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA SAYANSI YA HALI YA HEWA MASHULENI

Mkurugenzi wa Utafiti na matumizi wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a akitoa elimu ya sayansi ya hali ya hewa katika shule ya msingi ya Mount Evarest - Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Utafiti na matumizi wa TMA Dkt. Ladislaus Chang'a akitoa elimu ya sayansi ya hali ya hewa katika shule ya msingi ya Mother of Mercy - Dar es salaam.

Wanafunzi wakipokea zawadi mbalimbali mara baada ya kufanya vizuri katika mitihani ya majaribio waliyopatiwa. 
Wataalam kutoka TMA wakisimika kituo cha kupima mvua (Raingauge) katika shule hizo

Wednesday, October 16, 2019

MHESHIMIWA ISSA HAJI USSI GAVU AITAKA TMA KUONGEZA MBINU ZA KUFIKISHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA WAKULIMA KWA WAKATI.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe. Issa Haji Ussi Gavu akipata elimu kutoka kwa mtaalamu wa hali ya hewa ya namna taarifa za hali ya hewa zinavyoweza kusaidia kukuza sekta ya kilimo hapa nchini kupitia maonesho ya siku ya chakula duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe. Issa Haji Ussi Gavu akitoa maelekezo mara baada ya kupata elimu kutoka kwa mtaalamu wa hali ya hewa kupitia maonesho ya siku ya chakula duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe. Issa Haji Ussi Gavu akipokea zawadi toka kwa meneja wa hali ya hewa kituo cha Pemba Bi. Bishara Mdowe kupitia maonesho ya siku ya chakula duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019


Tarehe 14/10/2019 Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe. Issa Haji Ussi Gavu aliwataka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuongeza mbinu za kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wakulima kwa wakati, alizungumza hayo alipotembelea banda la TMA lililopo kwenye maonesho ya siku ya chakula duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.                                                     
“Ninawataka muongeze mbinu za kuhakikisha taarifa zenu zinawafikia wakulima kwa wakati”  alisisitiza Mhe. Issa 

Aidha, Mheshimiwa Issa ameipongeza TMA kwa juhudi kubwa inayoifanya na kufanikiwa kuongeza usahihi wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini. Maonesho hayo yamefungwa rasmi Tarehe 15 Oktoba 2019 na makamu wa pili wa Rais, baraza la mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.

Monday, October 14, 2019

TMA YAHIMIZA WAKAZI WA PEMBA KUTUMIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA SEKTA YA KILIMO.



Meneja wa hali ya hewa kituo cha Pemba Bi. Bishara Mdowe akiendelea kutoa elimu ya hali ya hewa na kuwakaribisha wakazi wa Pemba kutembelea banda la hali ya hewa kupitia vyombo vya habari kwenye maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe, kisiwani Pemba kuanzia Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.

Afisa mdhamini Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Usafirishaji Pemba ndugu. Hamad Baucha akipata elimu kutoka kwa mtaalamu wa hali ya hewa ya namna taarifa za hali ya hewa zinavyoweza kusaidia kukuza sekta ya kilimo kupitia maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe, kisiwani Pemba kuanzia Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.














Matukio mbalimbali katika picha wakati wataalamu wa hali ya hewa kutoka TMA wakiendelea kutoa elimu ya namna taarifa za hali ya hewa zinavyoweza kusaidia katika kukuza sekta ya kilimo kupitia maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe, kisiwani Pemba kuanzia Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.



Wanafunzi wakipokea zawadi mbalimbali mara walipotembelea banda la TMA kupitia  maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe, kisiwani Pemba kuanzia Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019.

Kuanzia tarehe 10  hadi 16 Oktoba 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inashiriki katika maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba, ambapo wataalamu wa hali ya hewa wameendelea kutoa elimu kwa wakazi kisiwani Pemba juu ya umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta ya kilimo. 


Meneja wa hali ya hewa kituo cha Pemba Bi. Bishara Mdowe aliongea na wananchi wa Pemba kupitia vyombo vya habari na kuwakumbusha kuwa hivi sasa dunia imekumbwa  na mabadiliko ya tabia nchi, hivyo kuwataka kuhacha kufanya shughuli za kilimo kwa mazoea ili kuepusha hasara zisizo za lazima na badala yake waanze kutumia taarifa za hali ya hewa ili kufanya kilimo chenye tija kitakachokuza uchumi wao pamoja na Taifa kwa ujumla.      
    “Ninawakumbusha wananchi wa pemba, hivi sasa Dunia imekumbwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo tuache kufanya shughuli za kilimo kwa mazoea, ninawahimiza kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuepusha hasara zisizo za lazima”.


Aidha kwa upande wa wageni waliotembelea katika  banda la TMA lililopo katika maonesho hayo akiwemo afisa mdhamini Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Usafirishaji Pemba ndugu Hamad Baucha walionesha kufurahishwa na namna elimu inavyotolewa na kuomba elimu iendelee kutolewa mara kwa mara zaidi kupitia vipindi vya redio na runinga. Kauli mbiu ya maonesho hayo ni "Matendo yetu ndiyo Hatma yetu, Lishe Bora kwa Ulimwengu usio na Njaa"

Friday, October 11, 2019

TMA YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA ZA MSIMU MARA MOJA KWA MWAKA.




Dar es Salaam,Tarehe 10/10/2019: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za mwaka (Novemba 2019 hadi Aprili 2020) na athari zinazoweza kujitokeza. Utabiri huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka ikiwa ni mikoa ya Kigoma, Tabora,Rukwa,Katavi,Mbeya, Songwe, Njombe,Iringa, Lindi, Dodoma, Singida, Mtwara na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa WMO Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo kwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika kwa vile maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na mvua za kutosha.
‘Naendelea kutoa rai kwa wananchi wa mikoa husika kuzitumia mvua hizi kwa kupanda mazao sahihi kwa kufuata ushauri wa wataalamu, kama tunavyoona maeneo mengi yatarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani’, alisema Dkt. Kijazi.

Aidha, Dkt. Kijazi alifafanua kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi kwa kusema kuwa mvua hizi ni za msimu wa vuli kwa maeneo yanayopata mvua mbili kwa mwaka na katika kipindi hiki cha vuli kunatarajiwa kuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa ambapo alimalizia kwa kuwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA sambamba na kuchukua tahadhari ya vipindi vifupi vya mvua kubwa,upepo mkali na mawimbi makubwa, vinavyotarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo.

Utabiri uliotolewa kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka unaonesha maeneo ya mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Rukwa Kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara, yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani na maeneo ya mikoa ya Kigoma na Katavi,  yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Wednesday, October 9, 2019

WANAHABARI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUFIKISHA HABARI ZA HALI MBAYA YA HEWA KWA WAKATI.

Wanahabari katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza.
Wadau katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza.
Mmoja wa wadau akichangia mada wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza.

Tarehe 09/10/2019: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau wa sekta mbalimbali na wanahabari ili kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kusambaza taarifa za hali ya hewa ukiwemo utabiri wa hali ya hewa na tahadhari ya hali mbaya ya hewa, huku akitolea mfano wa athari zilizoanza kuonekana mwanzoni mwa msimu wa mvua za vuli za mwaka huu.

“Napenda kusisitiza umuhimu wa warsha hizi ni kuhakikisha jamii tunayoenda kuihudumia inapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka kirahisi, msimu wa vuli umeanza na matukio mengi ya upepo mkali, mawimbi makubwa na mvua kubwa hivyo taarifa hizi zinakuwa na manufaa pale ambapo zinatumika kwa wakati’, alisema Dkt. Kijazi. Aidha, alivishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kusambaza kwa wakati taarifa za hali ya hewa ikiwa pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa.  

Kwa upande mwingine, Dkt.Kijazi alifafanua kwa wadau wa sekta mbalimbali sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya 2019. Alisema lengo la Sheria hiyo ni kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini na kutoa mwongozo wa ushiriki wa sekta mbalimbali  katika matumizi ya huduma hizo. Dkt. Kijazi alifafanua vipengele vya sheria hiyo vinavyowahusu wadau wa huduma za hali ya hewa alipokuwa anafunga mkutano huo wa wadau.

Aidha, wadau hao walipata fursa ya kutoa ushauri wa athari zinazoweza kujitokeza kulingana na utabiri wa msimu wa mwaka ulioandaliwa kwa mikoa inayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ambayo ni  mikoa ya kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Kwa upande wa wanahabari waliahidi kuendelea kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na waliishukuru TMA kwa kuendesha warsha hizo ambazo zimeendelea kuwajengea uwezo wa kuelewa lugha inayotumika katika utabiri wa hali ya hewa.

 Warsha hizo zilifanyika tarehe 08/10/2019 kwa kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali na tarehe 09/10/2019 kwa kuwakutanisha wanahabari. Utabiri wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 unatarajiwa kutolewa rasmi kwa umma kupitia vyombo vya habari siku ya Alhamisi, tarehe 10/10/2019,makao makuu ya ofisi za TMA, saa tano kamili asubuhi.

TMA YAJIPANGA KUTOA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA MWAKA KWA MWEZI NOVEMBA 2019 HADI APRILI 2020 KWA KUWANOA WANAHABARI

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi akifafanua jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) katika warsha ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 katika ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza Dar es Salaam, Tarehe 09 Oktoba 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi katika picha ya pamoja na wanahabari walioshiriki warsha ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 katika ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza Dar es Salaam,Tarehe 09 Oktoba 2019.
Wanahabari mbalimbali wakichangia mjadala katika warsha ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 katika ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza Dar es Salaam,Tarehe 09 Oktoba 2019.
Mtaalamu wa hali ya hewa Bw. Abuubakar Lungo akifafanua jambo kwa kina kwa mwanahabari kutoka gazeti la habari leo Bi. Theopista Nsanzugwako katika warsha ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 katika ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza Dar es Salaam,Tarehe 09 Oktoba 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi akifunga rasmi warsha ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 katika ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza Dar es Salaam,Tarehe 09 Oktoba 2019.
Utabiri wa msimu wa mvua za mwaka kwa mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zake utatolewa rasmi siku ya Alhamis,Tarehe 09 Oktoba 2019, Ofisi za TMA, Ubungo Plaza, Dar es Salaam

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...