Monday, August 28, 2023

MRADI WA UJENZI WA OFISI YA TMA, KANDA YA MASHARIKI NA KITUO CHA KUTOA TAHADHARI ZA TSUNAMI NCHINI WAKAGULIWA



Dar es Salaam;Tarehe 28 Agosti, 2022;

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Kanda ya Mashariki na Kituo cha kutoa tahadhari za TSUNAMI nchini, unaotekelezwa katika maeneo ya SIMU 2000, Jijini Dar es Salaam. 

Mradi huo ambao utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 9 za kitanzania, unatarajiwa kukamilika mwezi Julai,2024. Akizungumza wakati wa ziara yake, Dkt. Nyenzi alisema, chini ya Serikali ya Awamu wa Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mamlaka imekuwa wanufaika wakubwa katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini ukiwemo mradi huo ambao utahusika moja kwa moja katika utoaji wa tahadhari za TSUNAMI nchini na hivyo kuongeza tija katika mipango ya nchi. 

Aidha, Dkt. Nyenzi alifurahishwa na kasi ya ujenzi unavyoendelea kutokana na hatua mbalimbali ambazo mkandarasi amezichukua ikiwa ni pamoja na kufanya kazi muda wa ziada na kuongeza nguvu kazi ili kuhakikisha makubaliano ya kimkataba yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati. Dkt. Nyenzi alisisitiza matumizi ya malighafi zenye ubora na kutoa fursa za ajira kwa wazawa katika mradi huo.

Thursday, August 24, 2023

VULI 2023: MVUA ZA JUU YA WASTANI HADI WASTANI ZINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang'a akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha Utabiri wa Mvua za Msimu wa VULI (Oktoba hadi Disemba 2023), katika ukumbi wa Emerald, Ubungo Plaza - Tarehe 24 Agosti 2023.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshirikia katika utoaji wa Utabiri wa Mvua za Msimu wa VULI (Oktoba hadi Disemba 2023), katika ukumbi wa Emerald, Ubungo Plaza - Tarehe 24 Agosti 2023.


Dar es Salaam; Tarehe 24 Agosti, 2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023. Aidha, maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), katika ukumbi wa Ubungo Plaza,Dar es Salaam,Tarehe 24 Agosti 2023. Alifafanua kuwa kutokana na uwepo wa El-NiƱo, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini, hata hivyo, mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi. “Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023. Kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023”. Alisema Dkt. Chang’a.

 Dkt. Chang’a alitoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa24, siku 10, mwezi natahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.

 Akimaliza kutoa taarifa hiyo, Dkt. Chang’a alisema, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.

Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.


Wednesday, August 23, 2023

WANAHABARI WASISITIZWA KUSAMBAZA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA WAKATI NA USAHIHI.

Mgeni rasmi ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang'a akiwa katika picha ya pamoja na washiriki  wa warsha ya wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba), uliofanyika katika Ukumbi wa TARI, Kibaha - Pwani, Tarehe 23 Agosti, 2023.


Mgeni rasmi ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang'a akizungumza na wanahabari alipokuwa akifungua warsha ya wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), uliofanyika katika Ukumbi wa TARI, Kibaha - Pwani, Tarehe 23 Agosti, 2023

Kaimu Meneja Masoko na Uhusiano -TMA, Bi. Monica Mutoni akiwasilisha Mada katika warsha ya wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), uliofanyika katika Ukumbi wa TARI, Kibaha - Pwani, Tarehe 23 Agosti, 2023.




Matukio mbalimbali kwa picha wakati washiriki kutoka vyombo mbalimbali vya habari  wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kupitia warsha ya wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), uliofanyika katika Ukumbi wa TARI, Kibaha - Pwani, Tarehe 23 Agosti, 2023



Monday, August 7, 2023

MHE. MIZENGO PINDA ATEMBELEA BANDA LA TMA











Mbeya; Tarehe 07 Agosti, 2023;

Waziri Mkuu Mtaafu wa Awamu ya nne, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ametembelea banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) lililopo katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya, kupitia maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kufanyika kuanzia Tarehe 01 hadi 08 Agosti 2023.

Mhe. Pinda akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Ndg. Gerald Musabila Kusaya amepata elimu ya hali ya hewa kutoka kwa Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo Ndg. Isack Yonah na kujionea namna kifaa chenye Teknolojia ya kisasa kinavyopima taarifa mbalimbali za hali ya hewa.

Aidha, kupitia maonesho hayo wadau pamoja na wanafunzi mbalimbali wameendelea kumiminika katika banda hilo ili kujifunza na kupata ufafanuzi wa taarifa mbalimbali zinazotolewa na TMA.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...