Friday, October 30, 2020

TMA YAENDELEA KUJIPANGA KUTOA UTABIRI KWA MAENEO MADOGO MADOGO YA NCHI.

Dar es salaam, Tarehe 23/10/2020 “Tunaendelea kujipanga ili tuje kutoa utabiri wa maeneo madogo madogo, katika ngazi ya Wilaya, Tarafa na hata Kata”, aliongea hayo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alipokuwa akifungua kikao kazi kilichowakutanisha wataalam wa TMA pamoja na maafisa Ugani kutoka katika wilaya ya Kilolo – Iringa, Kongwa – Dodoma, Ruangwa – Lindi na Uyui – Tabora ili kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Novemba 2020 – Aprili 2021 kwa maeneo madogomadogo katika ngazi ya Wilaya kilichofanyikia Tarehe 23 Oktoba 2020 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya Tatu- Ubungo plaza. Aidha, Dkt. Kijazi aliwasisitiza maafisa ugani mara watakaporudi katika maeneo yao ya kazi kupeleka elimu hiyo ya hali ya hewa waliyoipata kwa wananchi ili waweze kutumia vyema utabiri wa hali ya hewa katika shughuli zao za kilimo. Alieleza kwamba wapo baadhi ya wananchi wanaotumia utabiri wa asili (Indigenous knowledge), hata hivyo utabiri huo katika kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na mabadiliko ya tabia nchi unakuwa si wa kutegemea, ni vyema kufuatilia utabiri unaotolewa na TMA ambao umejikita katika uchambuzi wa mifumo ya kisayansi. Kwa upande wa wadau wakitoa mrejeo wa utabiri wa msimu wa mvua za Novemba 2019 – Aprili 2020 kwa maeneo madogomadogo katika ngazi ya Wilaya, waliipongeza TMA kutokana na utabiri kwenda sawa na kile kilichotokea katika maeneo yao. Aidha waliishukuru TMA kwa elimu muhimu waliyopata kupitia kikao kazi hicho, ambayo wameahidi kuifikisha kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi ili kusaidia kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo.

JARIDA LA HABARI TOLEO LA 6.

Kwa taarifa zaidi tembelea: www.meteo.go.tz

Wednesday, October 21, 2020

TMA IMETOA RASMI MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA ZA MSIMU MARA MOJA KWA MWAKA.

Dar es Salaam,Tarehe 21/10/2020: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ikijumuisha mikoa iliyopo magharibi mwa nchi ( Kigoma, Tabora na Katavi), nyanda za juu kusini magharibi (Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa), katikati mwa nchi (Dodoma na Singida), pwani ya kusini (Lindi na Mtwara), mkoa wa Ruvuma pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro na pia kuelezea athari zinazoweza kujitokeza. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika. ‘Naendelea kuwahimiza wananchi waishio katika mikoa husika kuhifadhi mazao baada ya kuvuna kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam ili kuepuka uharibifu unaoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua na unyevunyevu inayotarajiwa kwani maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani’ alisema Dkt. Kijazi. Kuhusu mvua za msimu wa Vuli kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ilielezwa kuwa zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo alisisitiza kuwa mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari 2020. Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka utabiri ulionesha katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, Kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani huku mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi mvua zikitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani. Dkt. Kijazi aliendelea kuelezea kuwa mvua hizo kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajiwa kuanzia mkoa wa Tabora katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 na baadae kutawanyika katika mikoa mingine ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 na ikitarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya nchi katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, japo kwa mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuisha katikati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021. Kwa taarifa zaidi tembelea:

Tuesday, October 20, 2020

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI TMA IKIJUMUIKA NA WANAHABARI KATIKA KUJADILI UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA VULI KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MOJA KWA MWAKA ( NOVEMBA 2020 HADI APRILI 2021) UNAOTARAJIA KUTOLEWA RASMI TAREHE 21 OKTOBA 2020.

DKT. NYENZI ATOA RAI KWA WADAU KUSHIRIKIANA NA TMA KATIKA KUELIMISHA WANANCHI, UMUHIMU WA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

Dar es Salaam, Tarehe; 19/10/2020. Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia alikuwa ni mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa maandalizi ya kutoa utabiri wa mvua za msimu wa vuli kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka Dkt. Buruhani Nyenzi ametoa rai kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kushirikiana na TMA katika kuelimisha wananchi ikiwemo watendaji kutoka katika sekta zao juu ya umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zao za kila siku, aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa TMA, Makao Makuu - Ubungo Plaza, Dar es salaam, Tarehe 19 Oktoba 2020. “Ninatoa rai kwenu wadau kushirikiana na TMA katika kuelimisha wananchi ikiwemo watendaji kutoka katika sekta zenu, juu ya umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zao za kila siku ili kuepusha au kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa sambamba na kulinda mafanikio ya uwekezaji na miundombinu iliyofanywa na Serikali”. Alisisitiza Dkt. Nyenzi. Katika hotuba yake Dkt. Nyenzi aliwakumbusha wadau kuwa maboresho yaliyofanywa na TMA yamesababisha kutoa utabiri wenye viwango vya usahihi uliofikia asilimia 94.4% kwa msimu wa mvua za Novemba 2019 hadi Aprili 2020, kiwango ambacho kimezidi kiwango kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70%, ambapo aliishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuiwezesha TMA mpaka kufikia mafanikio hayo. Pia katika hotuba yake alitoa pole kwa wananchi wote walioguswa na maafa yaliyotokana na mvua kubwa iliyotokea Tarehe 13 na 15 Oktoba, 2020 na kuomba washiriki kusimama kwa dakika moja kama ishara ya kuwakumbuka wale waliofariki kutokana na maafa hayo. Pia alieleza kuwa kwa hivi sasa taarifa za hali ya hewa zikitumika ipasavyo katika sekta mbalimbali itasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazotosheleza uendeshaji wa viwanda vyetu, hivyo kusaidia kufikia malengo ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda. Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwashukuru wadau kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinatumika katika sekta zao na kuwashukuru kwa kushiriki vikao vya wadau ambavyo vinafanyika kila mara unapotolewa utabiri wa msimu. Aidha, wadau walioudhuria mkutano huo, waliipongeza TMA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa utabiri ambao kwa kiwango kikubwa umekuwa na uhalisia na kuahidi kuendelea kutumia utabiri unaotolewa na TMA katika kupanga mipango yao ya kiutendaji na ya maendeleo katika sekta zao. Walisema utabiri uliopita ulikuwa wa manufaa sana katika sekta zao na umesaidia kupunguza hasara ambazo zingetokea endapo utabiri usingetumika.

Tuesday, October 13, 2020

MWENENDO WA MVUA KWA UKANDA WA PWANI YA KASKAZINI

Dar es Salaam, 13 Oktoba 2020: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inapenda kutoa ufafanuzi juu ya uwepo wa vipindi vya mvua zinazoendelea leo katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba). Mvua hizo zimetokana na uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la bahari ya Hindi uliosababisha kuvuma kwa upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya pwani ya nchi yetu. Hata hivyo, mvua hizi ni za muda mfupi na zinatarajiwa kupungua kwa siku ya kesho tarehe 14 Oktoba, 2020 na kuongezeka kidogo tarehe 15 Oktoba, 2020. Aidha, mvua za Vuli (Oktoba-Disemba, 2020) katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 kama zilivyotabiriwa hapo awali (Septemba, 2020) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hiyo katika bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi. USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

MIAKA 21 KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE


 

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...