Saturday, January 20, 2024

VIPINDI VYA MVUA KUBWA KATIKA BAADHI YA MAENEO NCHINI


 ​Dar es Salaam, 20 Januari, 2024:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya vipindi vya mvua kubwa vilivyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.

Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini zimepelekea uwepo wa athari katika baadhi ya maeneo. Mnamo usiku wa tarehe 19 kuamkia tarehe 20 Januari, 2024 vimejitokeza vipindi vya mvua kubwa zilizoambata na upepo mkali katika baadhi ya maeneo nchini na kusababisha athari ikiwemo mafuriko, uharibifu wa mali na miundombinu. Maeneo yaliyokumbwa na mvua hizo ni pamoja na Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Kilimanjaro na Manyara pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba. Hadi kufikia saa 3 asubuhi ya leo (20 Januari, 2024) kituo cha Zanzibar kiliripoti kiasi cha milimita 85.2 za mvua kwa saa 24 ikifuatiwa na kituo cha Kibaha milimita 84.8 na Dar es Salaam milimita 54.6.

Uwepo wa mvua hizo unasababishwa na kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa inayosababisha mvua nchini ikiwemo hali ya El-NiƱo kama ilivyoelezwa hapo awali. Aidha, Ukanda Mvua pamoja na kuimarika kwa migandamizo midogo ya hewa iliyopo mashariki mwa kisiwa cha Madagascar imepelekea pia kuwepo na vipindi vya mvua kubwa. Migandamizo hiyo midogo ya hewa inapelekea kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka magharibi (Misitu ya Kongo) kuelekea baadhi ya maeneo ya nchini. Aidha, katika taarifa za mwelekeo wa mvua za Vuli, 2023 iliyotolewa tarehe 24 Augusti, 2023 na Mvua za Msimu 2023/2024 iliyotolewa tarehe 31 Oktoba, 2023 zilionesha uwepo wa vipindi vya mvua za nje ya msimu katika kipindi cha miezi ya Januari na Februari, 2024 hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa bado unaendelea kuonesha uwepo wa hali hiyo ya vipindi vya mvua vya nje ya msimu. Mamlaka inaendelea kufuatilia mienendo ya hali ya hewa nchini na kutoa mrejeo pale itakapobidi. Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Wednesday, January 17, 2024

Chair) katika Mkutano wa 60 wa IPCC (IPCC-60)



Mojawapo ya majukumu ya TMA ni kuwakilisha Tanzania Kikanda na Kimataifa katika Masuala ya Hali ya Hewa. Pichani ni Dkt. Ladislaus Chang'a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu (TMA) na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi -IPCC (IPCC-Vice Chair) katika Mkutano wa 60 wa IPCC (IPCC-60), Instanbul, Uturuki, tarehe 16-19 Januari 2024.

Friday, January 12, 2024

KATIBU MKUU UCHUKUZI ATOA RAI CHUO CHA HALI YA HEWA KUANZISHA SHAHADA.


 



Zanzibar; Tarehe 11/01/2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara ametoa rai kwa Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma (NMTC) kuanzisha Shahada ya Sayansi ya Hali ya Hewa (Bsc. in Meteorology) ili kumrahisishia mwanafunzi anayetaka kujiunga katika ngazi ya Stashada (Diploma) kujiendeleza zaidi hadi hatua ya Shahada chuoni hapo, alisema hayo alipotembelea Banda la TMA lililopo katika maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 60 Matukufu ya Mapinduzi ya Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho ya Biashara, Nyamanzi, Mjini Magharibi, Zanzibar kuanzia tarehe 07 - 19 Januari, 2024.

"Kupitia Chuo chenu cha hali ya hewa Kigoma mfanye uwezekano wa kutoa elimu hiyo ya hali ya hewa mpaka ngazi ya degree ili kumrahisishia mwanafunzi anayetaka kujiunga katika ngazi ya Stashada atarajie wepesi wa kujiendeleza zaidi hadi hatua ya Shahada chuoni hapo". Alisisitiza Prof. Kahyarara

Awali Kaimu Meneja wa Masoko na Uhusiano Bi. Monica Mutoni alifafanua kuwa kwa sasa Stashahada ya sayansi ya hali ya hewa (Bsc. in Meteorology) inatolewa katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Stashahada ya Uzamili (PGD). Aidha, aliishukuru serikali kwa uboreshaji mkubwa unaoendelea kufanyika kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Zanzibar, ambaye ni Mtaalamu Mwandamizi wa Hali ya Hewa Bw. Hassan Ame alielezea namna TMA Zanzibar ilivyojipanga katika kuwahudumia wadau wake akisema kwa upande wa Kilimo kuna vituo viwili vinavyowahudumia wadau wa kilimo kimoja kipo Matangatuani, Pemba na kingine Kizimbani, Unguja. Kwa wateja wa bandarini alisema wanahudumiwa na kituo cha Malindi, Unguja pamoja na bandarini Mkoani, Pemba. Katika ufafanuzi wake alielezea namna TMA inavyoshirikiana na Taasis nyingine ikiwemo Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa (ZDMC), Mamlaka inayohusika na masuala ya usafiri wa Baharini (ZMA) pamoja na Mamlalaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Thursday, January 11, 2024

HERI YA MIAKA 60 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR


 

WANANCHI WAFURAHISHWA NA ELIMU YA HALI YA HEWA, ZANZIBAR.

 








Zanzibar; Tarehe 10/01/2024

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Zanzibar, wamefurahishwa na elimu ya hali ya hewa inayotolewa katika maonesho ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho ya Biashara, Nyamanzi, Mjini Magharibi, Zanzibar kuanzia Tarehe 07 - 19 Januari, 2024.

Wageni mbalimbali waliweza kutembelea banda la TMA wakiwemo viongozi wa Taasis za serikali zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Prof. Ulingeta Mbamba, Shirika la Reli Tanzania Bw. Masanja Kadogosa, Mkurugenzi wa Huduma za Taasis kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Hamidu Mbegu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bw. Teophoy Mbilinyi ambao waliipongeza TMA kwa huduma nzuri ya usahihi wa Utabiri inayotolewa .

Aidha, wataalam wa hali ya hewa kutoka TMA wameendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kutumia huduma mahususi zinazotolewa na TMA pamoja na kuelewa namna ya kutumia taarifa za hali ya hewa kwa usahihi ili kukabiliana na athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...