Friday, April 17, 2020

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MWONEKANO WA ANGA KUWA NA RANGI NYEKUNDU AU CHUNGWA KATIKA BAADHI YA MAENEO NCHINI.



Dar es Salaam, 17 Aprili 2020:

Kumekuwa na hali ya taharuki na maswali kutoka kwa umma terehe 16 Aprili, 2020 jioni kuhusu mwonekano wa anga kuwa na rangi nyekundu au chungwa katika baadhi ya maeneo nchini.  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa ufafanuzi kuhusu hali hiyo ya anga kama ifuatavyo;
Mwonekano huo wa rangi ya anga ni hali ya kawaida ambayo hutokea wakati jua linapozama au kuchomoza katika mazingira yenye kuwa na hali ya hewa kama vile mawingu, matone madogo madogo ya maji na barafu katika anga mara mvua inapokatika na jua linapokuwa katika upande tofauti na eneo mvua inaponyesha. Hali ambayo husababisha kutawanywa kwa miale ya mwanga wa jua. Hivyo kutokana na ukubwa wa matone ya maji katika wingu na chembechembe za vumbi katika anga, sehemu ya miale ya jua inayotawanywa zaidi katika mazingira hayo ni mawimbi ya miale ya jua inayohusiana na rangi nyekundu au chungwa hivyo kufanya anga kuonekana katika rangi hizo (Mawimbi madogo sana huwakilisha rangi ya blue na makubwa rangi nyekundu au rangi ya chungwa). Hali hii haina tofauti sana na namna Upinde Mvua unavyojitokeza angani, isipokuwa upinde mvua unakuwa na rangi zote saba za spectrum ya mwanga.  Mabadiliko hayo ya hali ya anga hayana madhara yeyote.

Katika hali iliyozoeleka mara nyingi, anga huonekana kuwa rangi ya bluu kutokana na kutawanywa kwa mawimbi ya miale ya jua kunakofanywa na gesi ya Nitrojeni na Oksijeni ambazo ndizo hufanya sehemu kubwa ya gesi katika hewa. Hali hiyo inatokana na molekuli za gesi hizo kuwa ni ndogo sana hivyo hutawanya sehemu ya mawimbi madogo zaidi ya miale ya jua iliyo katika rangi ya blue katika spectrum ya mwanga. Rangi hiyo huonekana katika macho ya binadamu kwa kipindi hicho.

Wednesday, April 8, 2020

DKT. KIJAZI: MWAKA 2019 ULIREKODI KIASI CHA MVUA NYINGI TANGU MWAKA 1970.



Dar es Salaam, Tarehe 08/04/2020:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa ripoti ya tathimini ya hali ya hewa ya Tanzania kwa mwaka 2019. Uzinduzi wa ripoti hiyo ulifanyika wakati wa kikao cha Bodi ya TMA kilichofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TMA.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alisema mwaka 2019 umechukua nafasi ya nne kwa kurekodi kiasi cha mvua nyingi tangu mwaka 1970.

 Kiwango cha mvua nchini kwa mwaka 2019 kilikuwa ni wastani wa milimita 1283.5 sawa na asilimia 125 ya wastani wa mvua ya muda mrefu (1981-2010), kiwango hiki ni zaidi ya wastani wa mvua ya muda mrefu kwa milimita 256.5. Katika historia, mvua hii imechukua nafasi ya nne kwa wingi kati ya miaka iliyopata mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ambapo miaka iliyokua na mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ni 1982, 1997 na 2006”. Alisema Dkt. Kijazi

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa joto la nchi limeendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu kuanzia mwaka 1995, ambapo joto la usiku limeongezeka zaidi ilikilinganishwa na joto la mchana. Pamoja na hayo taarifa za ripoti zitolewazo zimekuwa zikichangia ripoti za tathimini ya hali ya hewa ya dunia zinazoandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Vilevile Dkt. Kijazi alitoa wito kwa wadau wa sekta mbalimbali kutumia taarifa zilizopo kwenye ripoti hiyo kwaajili ya mipango ya maendeleo ya kiuchumi na jamii kama vile kilimo, ujenzi, maendeleo ya viwanda n.k

Awali wakati akitoa maelezo ya jumla, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema kuwa, ripoti hizi zimekuwa zikitolewa tokea mwaka 2011 hadi 2019 na lengo ni kukuza ufahamu na uelewa kwa jamii, wadau na watoa maamuzi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi. “Tathmini za ripoti hizi huonesha taarifa za kina za uchambuzi wa hali ya hewa na athari zake na kuziweka katika mtazamo wa kihistoria”. Alisema Dkt. Chang’a
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Buruhani Nyenzi aliipongeza Menejimenti ya TMA kwa kutoa taarifa hiyo kwani ilielezwa kwamba ni nchi mbili tu Afrika ambazo zinatoa taarifa hizo ikiwemo Tanzania na Ivory Coast

Monday, April 6, 2020

KARUME DAY


TMA inaungana na watanzania wote kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 48 ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais wa  Tanzania.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...