Monday, March 23, 2020

UJUMBE WA DKT. AGNES KIJAZI MKURUGENZI MKUU WA TMA NA MAKAMU WA TATU WA RAIS WA WMO KATIKA WMD 2020.

Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi la siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila Nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za Hali ya Hewa za nchi husika. Taasisi hizo hutumia siku hii kuonyesha na kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.
Kwa hapa nchini kwetu Tanzania, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). TMA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kabla ya hapo taasisi hii ilikuwa ni wakala wa serikali.

Katika kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”. Kaulimbiu hii inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji.
Kwa kawaida maji yapo katika hali mbalimbali ambazo ni yabisi (barafu), kimiminiko (maji ya kawaida) na gesi (mvuke). Hali hizo zinatokana na mzunguko ambao maji hupitia ujulikanao kama hydrological cycle unaohusisha ardhi, anga, bahari, maziwa, misitu na mazingira mengine. Ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari, mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso wa dunia. Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji. Changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kupelekea upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ni ongezeko la kina cha bahari Duniani kote. Hii husababishwa na mambo makubwa mawili: kwanza, ni kutanuka kwa maji ya bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji, na pili ni kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika. Ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo ili kuyafanya bora na yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.

Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo.
Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate sensitive sectors) ikiwemo sekta ya maji.

Katika kutimiza mahitaji ya wadau na matakwa ya program ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA, Mamlaka ya Hali ya Hewa hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali ya hewa. TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye uso wa dunia nchi kavu (ground weather stations), vilivyopo bandarini (marine weather stations) na vilivyopo katika anga la juu ambavyo vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations).

Aidha, TMA hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwaajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi. Utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast), mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, zikiwa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi hali ya hewa na maji. Aidha, TMA hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji. Utabiri huu husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS).

TMA imeendelea kupata mafanikio zaidi katika kutekeleza mpango mkakati wake. Mafanikio hayo ni pamoja na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Huduma Bora “Quality Management System (QMS) na kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.

Katika eneo la vifaa vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Mkakati huu umelenga kuboresha vituo vyote vya hali ya hewa nchini ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ya hali ya hewa duniani, na pia kutekeleza mkataba wa Minamata (Minamata Convention) unaozitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kusitisha matumizi ya zebaki kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2020.

Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji jitihada za wadau wote wa huduma za hali ya hewa, wakiwemo wadau wa maendeleo “Development Partners (DPs)” ili kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za sekta maalumu na maeneo madogomadogo (downcaled information) na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani Kwa mwaka huu wa 2020, napenda kutoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu. Napenda pia kuwaomba wadau wote kutuunga mkono katika utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini na kupunguza athari kwa jamii na sekta ambazo zinaathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo sekta ya maji.

Mwisho, nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD) 2020 yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”

KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, MHE. MHANDISI ISACK KAMWELWE ATOA WITO KWA WADAU WOTE WA HALI YA HEWA.

Kila mwaka tarehe 23 Machi, Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization-WMO) ambalo lilianzishwa tarehe 23 Machi, 1950. Tanzania pamoja na wanachama wengine 192 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani inaungana na jumuiya ya kimataifa kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii pia hutumika kuonesha mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za hali ya hewa ikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuchangia maendeleo na kukuza ustawi wa jamii. Taasisi za Hali ya Hewa duniani kote hutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa ambazo ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao.

Katika kusherehekea siku ya hali ya hewa duniani, ni desturi kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kutoa kaulimbiu ya maadhimisho ya kila mwaka. Kwa mwaka huu wa 2020 kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water). Kaulimbiu hii inaelezea ukweli kwamba, hali ya hewa ina mchango mkubwa katika mtawanyiko, mgawanyo, ubora na matumizi ya rasilimali maji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile kilimo, nishati, mifugo na uvuvi. Pia kwa kuzingatia kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi pamoja na matukio ya hali mbaya ya hewa inayoambatana na mabadiliko hayo yanaathiri sana mzunguko wa maji wa Dunia pamoja na upatikanaji na ubora wa maji.

Kwa upande wa Tanzania, kama ilivyo kwa wanachama wengine wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ina jukumu la kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wa hali ya hewa ambao huchangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa rasilimali maji. Upatikanaji wa rasilimali maji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa na malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals-SDGs). Huduma za hali ya hewa ni muhimu katika malengo hayo hususani lengo Na. 7 (SDG7) ambalo linahusiana na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Tanzania inaendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoahuduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa. Hii ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalam ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwemo sekta ya maji. Mwaka 2019, Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya 2019. Sheria hii inaiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Pia sheria iliyounda Mamlaka ya Hali ya Hewa inaipa nguvu za kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Aidha, Sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo sheria hii imehakikisha uwakilishi, ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za kijamii.
Katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini, Serikali inaendelea kuijengea uwezo Mamlaka hii ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mfupi na muda mrefu (climate variability and change). Taarifa za hali ya hewa ni za muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Taarifa na huduma za hali ya hewa husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu na hivyo kuliandaa taifa vizuri katika kukabiliana na maafa yanayosababishwa na vipindi vya ongezeko au upungufu wa maji kama vile mafuriko na ukame. Mfano wa uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko ni pamoja na mvua kubwa zilizonyesha katika msimu huu na kuharibu miundominu ya usafiri ikiwemo miundombinu ya reli, barabara na madaraja. Hivyo, huduma za hali ya hewa zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo, maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati, ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli yakiwemo madaraja na uratibu wa maafa miongoni mwa sekta nyingine. Aidha, katika jitihada za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa TMA kwa kuboresha mtandao wa Taifa wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa data na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango ya maendeleo katika sekta hizo.

Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa, Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini. Kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Juamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo imeboresha utendaji wa TMA katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hatuna budi kutumia huduma hizi ili kuboresha shughuli zetu za kila siku na vilevile kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuboresha huduma hizi kwa siku zijazo.
Uwekezaji wa Serikali katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hususani katika kuboresha miundombinu ni pamoja na ununuzi wa Rada za hali ya hewa kwa lengo hilo hilo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Rada hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya ununuzi ambazo zitafungwaMtwara, Mbeya na Kigoma. Aidha, ili kukamilisha mtandao wa Rada zitahitajika Rada zingine mbili ambazo zitafungwa Dodoma na Kilimanjaro. Pia kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa huduma za hali ya hewa na changamoto zinazotukabili ambazo zinahitaji kutatuliwa, Serikali itaendelea kuwekeza ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa wataalamu na miundombinu huku tukihimiza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali zinazohusiana na zinazotumia huduma za hali ya hewa na rasilimali maji kwa lengo la kuendelea kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Vilevile kwa kuzingatia maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini, ni vyema kuongeza juhudi katika kutumia huduma hizi katika mipango ya sekta zote za kiuchumi na kijamii na utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji.

Katika kuadhimisha Siku hii ya hali ya hewa Duniani yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water), ninatoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka sekta zote za kiuchumi na kijamii zinazotumia au kuathiriwa na hali ya hewa pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanazitumia huduma za hali ya Hewa kwa maendeleo ya Taifa letu. Sekta ya maji izitumie huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango yao ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu. Aidha, tuendelee kuunga mkono juhudi za TMA katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na udhibiti kwa kuendelea kuwapa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wote wenye vituo vya hali ya hewa wanavinasajili TMA ili kwenda sambamba na matakwa ya sheria. Ushirikiano huo utaiwezesha TMA kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini.

Mwisho nachukua fursa hii kuwatakia wananchi wote pamoja na jumuia yote ya kimataifa maadhimisho mema na yenye mafanikio ya siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2020.

Thursday, March 19, 2020

MHE. NDITIYE AAGIZA BARAZA LA TMA KUANDAA MIONGOZO NA MAFANIKO YENYE TIJA KWA SERIKALI.

Mhe. Mhandisi. Atashasta Nditiye akihutubia Baraza la Wafanyakazi, TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Bi. Jane Kikunya, akitoa neno kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi wa Baraza la Wafanyakazi  TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi akizungumza katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Meneja Rasilimali Watu na msimamizi wa Divisheni ya Huduma Saidizi wa TMA, akitoa maelezo mafupi katika Baraza la Wafanyakazi  TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020.

Mwenyekiti wa TUGHE - TMA, Bi. Aurelia Mwakalukwa akiwasilisha taarifa ya TUGHE - Makao Makuu TMA katika Baraza la Wafanyakazi  TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mwenyekiti wa TUGHE – Zanzibar  Ndg. Awesi Kheri Awesi akiwasilisha Salamu za TUGHE - Zanzibar katika Baraza la Wafanyakazi  TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mwenyekiti kinamama Zanzibar  Bi. Zaituni Khamis akiwasilisha Salamu za kinamama Zanzibar katika Baraza la Wafanyakazi  TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mwenyekiti kinamama TMA - Makao Makuu, Bi. Zainab Gumbo akiwasilisha Salamu za kinamama wa TMA katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mfanyakazi bora wa TMA, Ndg. Kisumo Msangi kutoka kituo cha TMA - Arusha akizungumza katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mwakilishi toka TUGHE  akimtambulisha mfanyakazi bora wa TMA 2020 katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020



Watoa mada wakiwasilisha mada za mkataba mpya wa baraza na mkataba mpya wa hali bora kazini, Ukimwi na Korona katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi TMA, Ndg. Chuki Sangalugembe  akitambulishwa kwa ajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TMA, mara baada ya uchaguzi katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Katibu msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi TMA, Bi. Meklina Merchedez akitambulishwa kwa ajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TMA, mara baada ya uchaguzi katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020


Waalikwa wa Baraza la Wafanyakazi la TMA wanaotarajia kustaafu mwaka huu 2020 wakiaga wajumbe wa Baraza hilo katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Meza Kuu, wakati wa ufunguzi rasmi wa Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Meza Kuu, wakati wa uchaguzi wa mfanyakazi bora katika Baraza la Wafanyakazi TMA, lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020




Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TMA, wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika baraza  hilo lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TMA, wakiwakumbuka wajumbe wa Baraza hilo waliofariki katika baraza  hilo lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TMA, wakiimba wimbo wa mshikamano “ Solidarity Forever” kwa kutumia ishara ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Korona katika baraza  hilo lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020


Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la TMA katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi Mhe. Mhandisi. Atashasta Nditiye katika baraza  hilo lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020

Mjumbe wa Baraza, Meneja wa Kanda ya Nyanda za juu Kusini Ndg. Issa Hamad akiwasilisha maazimio ya Baraza la wafanyakazi wa TMA katika baraza  hilo lililofanyika Dodoma Tarehe 16 na 17 Machi, 2020


Dodoma, Tarehe: 16/03/2020;
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Mhandisi. Atashasta Nditiye ameagiza wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuandaa miongozo na mafanikio yenye tija kwa Mamlaka  na Serikali kupitia mijadala ya Baraza hilo.

Mhe. Mhandisi. Nditiye alitoa maagizo hayo wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) linalofanyika katika Ukumbi wa Takwimu, Dodoma, Tarehe 16 na 17 Machi 2020.

Hakikisheni kwamba mnaweka vyema vipaumbele vyenu, na kutimiza mambo ya msingi kwanza ili kukabiliana na tatizo la ufinyu wa bajeti lililopo”. Alisema Mhe. Mhandisi. Nditiye

Aidha Mhe. Naibu Waziri aliitaka Mamlaka kuharakisha upatikanaji wa kanuni ili sheria ianze kufanya kazi kurahisisha ufanisi wa majukumu ya  Mamlaka.
 Endeleeni kuboresha utabiri na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa wakati na kwa usahihi kwa jamii ya watanzania na wageni wanaotembelea nchini, kwa kusema hivi naamini michango yenu katika mkutano huu wa Baraza lenu la wafanyakazi, itatoa matokeo makubwa yatakayoendeleza sekta ya hali ya hewa nchini na pia kuliwezesha Taifa letu kusonga mbele kiuchumi na kimaendeleo”. Alisisitiza Mhe. Mhandsi. Nditiye.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kujumuika na wajumbe wa Baraza katika ufunguzi wa Baraza hilo na Wizara kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa iliyoonesha katika kuboresha muundo mpya wa Mamlaka unaolenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi..
“Uwepo wako umetupa nguvu na ari mpya katika kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho TMA imekuwa Mamlaka kamili”.Alieleza Dkt. Kijazi
Aliendelea kwa kumueleza kuwa Baraza la mwaka huu ni kwa mujibu wa mkataba mpya kati ya Menejiment na TUGHE na linajumuisha wajumbe 98 kutoka vituo mbali mbali vya hali ya hewa hapa nchini ikijumuisha viongozi na wawakilishi wa wafanyakazi.                                      
Kwa upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Bi Jane Kikunya alimuomba Mhe. Naibu Waziri kusaidia katika kutatua changamoto ya ufinyu wa bajeti kwa kuongeza zaidi bajeti kwaajili ya kusaidia uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa
Mkutano huo wa Baraza ulianza na elimu ya namna ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Korona katika maeneo yao ya kazi na jamii kwa ujumla.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...