Thursday, February 22, 2024

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2024 KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

 






Dar es Salaam; Tarehe 22, Februari 2024.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, tarehe 22/02/2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

“Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo mengi na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024, Aidha, aliongeza kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2024.” Alisema Dkt. Chang’a.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha TMA kufikia hatua ya kuongeza usahihi wa utabiri.

Dkt. Chang’a alisisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, huku akibainisha kuwa usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.

Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/news/tma-yatoa-utabiri-wa-msimu-wa-mvua-za-masika-2024-kwa-maeneo-yanayopata-mvua-mara-mbili-kwa-mwaka



Wednesday, February 21, 2024

TMA YAWANOA WANAHABARI KUELEKEA MASIKA 2024









Dar es Salaam; Tarehe 21, Februari 2024

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali kujadili kuhusu utabiri wa msimu wa Masika (Machi –Mei) 2024, unaotarajiwa kutolewa tarehe 22 Februari 2024. Utabiri huu ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba, Tanga, Kilimanjaro,Arusha, Manyara,Simiyu, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kaskazini mwa Kigoma. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dar es Salaam, Tarehe 21/2/2024.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi, Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, alisema “Mkutano huu ni mwendelezo wa sehemu ya ushirikishwaji wa wanahabari katika kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa”. 

Aidha aliendelea kusisitiza kuwa, uzingatiaji wa taarifa  za hali ya hewa, hususan tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu na mali zao na katika kuongeza tija na ufanisikatika kupanga na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika sekta za kilimo, ujenzi, Afya, Maji, Ulinzi, Usafiri (Anga, Maji na Nchi Kavu), Madini, Utalii, shughuli za Bandari nk..

Dkt. Chang’a alisema kwa kuzingatia umuhimu huo wa huduma za hali ya hewa nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi chake imeendelea na jitihada za kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini ikiwemo uwekezaji mkubwa katika miundo mbinu ya uangazi, uchakati wa data na utabiri, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 59J. Hivyo, aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo, hali inayochangia Mamlaka kuendelea kuboresha huduma zake. 

Naye Mwakilishi wa washiriki kutoka gazeti la Majira, Bi. Penina Malundo,  aliishukuru TMA kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa kwa waandishi wa habari  katika kuhakikisha wanaandika habari za hali ya hewa kwa ufanisi na uweledi ili wananchi waweze kuelewa. 

“Utoaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari umeweza kuongeza tija kwa wananchi kufuatilia taarifa hizo katika kufanya shughuli zao hususan za kijamii”. Alisema Bi. Penina.

Katika mkutano huu, wanahabari walipata fursa ya kuona utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2024 na kutoa michango yao juu ya namna sahihi ya usambazaji wa taarifa katika kipindi chote cha msimu.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...