Friday, March 22, 2024

TANZANIA YAWANOA WANAMIBIA MASUALA YA HALI YA HEWA




 


Namibia: Tarehe 18/03/2024.

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewanoa watumishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuwapatia mafunzo ya kuhakiki weledi wa wafanyakazi wote wanaofanya kazi za kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege. Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi za Hali ya Hewa Namibia kuanzia tarehe 04 hadi tarehe 18/03/2024, Windhoek, Namibia. 

Akizungumza wakati wa kufunga rasmi mafunzo hayo, Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Caesar Waitara aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuichagua Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzani kuendesha mafunzo hayo,  pamoja na uwepo wa taasisi nyingi za hali ya hewa barani Afrika. Aidha, alizitaka taasisi zote mbili kuongeza ushirikiano zaidi katika masuala mbalimbali kwa lengo la kunyanyua uchumi na maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini kwetu ikiwa ni pamoja na kufunga miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na  kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa urahisi kwa watumiaji wa taarifa hizo, pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma (QMS) na weledi wa wafanyakazi”. Alisema Mhe.Waitara. 

Aidha, alieleza kuwa Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzoni kabisa kufanikisha kupata cheti cha ubora wa kimatiafa cha “ISO 9001:2015” katika utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga. Kupitia mafanikio hayo, Tanzania kuipitia TMA imeweza kuzisaidia nchi zingine kama vile Nigeria, Libya, Saudi Arabia, Maldives na Lesotho katika masuala uanzishaji na utekelezaji wa mifumo ya utoaji huduma bora za hali ya hewa katika viwango vinavyotambulika kimataifa. 

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia, Bw. Elias Aiyambo, aliishukuru Serikali yake kwa kukubali maombi ya kufanya mafunzo hayo muhimu kwa nchi, vilevile aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mafunzo na kuomba ushirikiano huo uendelee baina ya nchi hizi mbili.  

Akitoa mrejesho wa mafunzo hayo kwa mgeni Rasmi, Mratibu wa mafunzo hayo na Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi Ubora wa Huduma za Hali ya Hewa TMA, Dkt. Geofrid Chikojo, alisema wamefanikiwa kutoa elimu kwa wafanyakazi 20 wanaofanya kazi katika viwanja 8 vya ndege pamoja na Makao makuu. Kati ya hao 19 walifanikiwa kufanya majaribio ya weledi ambao 17 waliweza kuthibitisha kuwa na weledi unaotakiwa. Dkt. Chikojo alitoa ushauri kwa Serikali ya Namibia kuwa na mpango wa kuhakikisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma na weledi inaendelea kuimarishwa na kuwatumia ipasavyo wafanyakazi waliopata vyeti vya weledi katika mafunzo yaliyofanyika.







Saturday, March 16, 2024

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA UWEKEZAJI MKUBWA SEKTA YA HALI YA HEWA










Mwanza; Tarehe 16 Machi, 2024


Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta hali ya hewa nchini wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na TMA ikiwemo rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza, Tarehe 16/3/2024.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Seleman Kakoso (MB) wakati wa majumuisho ya ziara hiyo kwa kuridhishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kupelekea nchi yetu kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kuihakikishia nchi uhakika wa huduma inayotolewa kwa manufaa ya Taifa letu. Aidha, kamati imeipongeza pia TMA kwa kuongeza ubora na usahihi wa utabiri ikiwemo wa mvua zilizoambatana na Elnino. Pongezi hizo zilipokelewa kwa niaba ya Serikali na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David M.Kihenzile (MB) ambaye aliongoza uongozi wa Wizara na TMA.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kakoso aliagiza uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ufanyike pamoja na maslahi bora ya watumishi. “Tunaiomba Serikali imarisheni Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ili kiweze kuandaa wataalamu watakaofanya kazi, pili lindeni wafanyakazi wa TMA kwa kuwapatia maslahi mazuri, msipofanya hivyo Serikali itakuwa inasomesha vijana wengi na baadaye wote wanaondoka kwasababu hawalipwi vizuri”. Alisema Mhe. Kakoso.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la KImataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha TMA kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

 

“Rada hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga ziwani,hali mbaya ya hewa,upepo mkali na kutoa tahadhari kwa wananchi hususani watumiaji wa ziwa Viktoria na kuboresha taarifa zinazotolewa na kuimairisha tija na usalama kwa watumiaji wengine wa taarifa za hali ya hewa kama sekta ya usafiri wa anga, ulinzi, kilimo,uvuvi na utunzaji wa misitu”. Alieleza Dkt. Changa.

 

Rada ya hali ya hewa iliyopo Mwanza, inauwezo wa kufanya uangazi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga,Kagera, Mara na eneo kubwa la ziwa vicktoria. Vilevile, rada hii ni moja ya uwekezaji mkubwa unaoendelea wa kukamilisha mtandao wa rada saba zenye teknolojia ya kisasa hapa nchini, ambapo rada tano zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya na Kigoma na rada mbili zitakazofungwa Kilimanjaro na Dodoma zikiendelea na mategenezo Marekani.  

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...