Dkt. Agnes Kijazi, akitoa mada kuhusu umuhimu wa
kuzijengea uwezo mamlaka za hali ya hewa katika nchi wanachama wa shirika la
hali ya hewa duniani.
|
Dkt. Agnes Kijazi,
akishiriki katika jopo la majadiliano kuhusiana na matukio ya hali mbaya ya hewa yanayojitokeza ikiwemo
vimbunga katika bahari.
|
Dkt. Agnes Kijazi,
akitoa mada kuhusiana na mahusiano ya masuala ya Jinsia na changamoto ya
mabadiliko ya hali ya hewa.
|
Dkt. Ladislaus Chang’a (kulia) akishiriki
katika majadiliano kuhusiana na maandalizi ya Ripoti ya sita ya tathmini ya
mabadiliko ya hali ya hewa inayotarajiwa kukamilishwa mwaka 2022.
|
Madrid, Hispania Tarehe 13/12/2019;
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeshiriki Mkutano wa 25 wa Kimataifa wa
Mabadiliko ya Hali ya Hewa (2019 United Nations Framework Convention on Climate
Change-UNFCCC-COP25) uliofanyika tarehe 02-13 Disemba 2019 nchini Hispania.
Pamoja na kutoa mchango na ushauri katika sayansi ya hali
ya hewa kwa ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano huo, TMA ilishiriki
pia katika mikutano iliyofanyika sambamba na Mkutano huo wa UNFCCC-COP25, Mkurugenzi
Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO),
Dkt. Agnes Kijazi, alishiriki kutoa
mada na baadae katika jopo la majadiliano kuhusiana na umuhimu wa kujenga uwezo
na kuimarisha huduma za hali ya hewa, hususan katika nchi zinazoendelea
sambamba na kuweka msisitizo wa kuhakikisha dunia inaongeza jitihada za kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya hali ya hewa katika maeneo ya bahari na yaliyo kandokando ya
bahari.
“Kumekuwa
na ongezeko la kina cha bahari, ongezeko kubwa la vimbunga kwa upande wa
Afrika, mfano kimbunga IDAI kilishosababisha vifo vya mamia ya watu na kuharibu
mazao na makazi ya watu katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi, hii inaonesha
kuwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ni halisia, ni vyema tukachukua
hatua stahiki sasa”. Alisema Dkt. Kijazi.
Kwa upande mwingine, Dkt Kijazi
alishiriki kutoa mada kuhusiana
na masula ya jinsia na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa. Dkt. Kijazi,
alisisitiza kuwa kuna tofauti kubwa ya namnna ambavyo mabadiliko ya hali ya
hewa yanawaathiri wanawake, watoto, wazee na wanaume. Wanawake, watoto na wazee
wanaathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa hasa katika nchi zinazoendelea
kutokana na nafasi na shughuli zao katika jamii. Dkt. Kijazi aliitaka jumuiya
ya kimataifa kufuata mfano wa Tanzania katika kutoa nafasi kwa wanawake katika
nafasi za maamuzi, ambapo Makamu wa Rais wa Tanzania ni mwanamke, Naibu Spika
ni mwanamke na akasema vilevile na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
ni mwanamke ambaye ni yeye mwenyewe.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi kutoka TMA alielezea
umuhimu wa kuimarisha uangazi na uboreshaji wa huduma za hali ya Hewa katika
bara la Afrika na nchi zinazoendelea pamoja na kushiriki katika jopo la
majadiliano kuhusiana na maandalizi ya ripoti ya sita ya tathmini ya mabadiliko
ya hali ya hewa duniani, ambapo tayari kuna ripoti maalamu tatu zimetolewa na
maandalizi yanaendelea kukamilisha ripoti kuu nne na zinatarajiwa kukamilika
mwaka 2022.
Aidha, TMA ilishiriki pia hafla
ya WMO ya kusaini ushirikiano na
washirika wa maendeleo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa
(Alliance for Hydromet). Hafla hiyo ilimshirikisha Katibu Mkuu wa WMO, Prof.
Petteri Taalas, viongozi mbalimbali wa WMO na viongozi wa Taasisi za Hali ya
Hewa-Afrika ikiwemo Malawi, Uganda na Tanzania.
No comments:
Post a Comment