Monday, May 11, 2020

SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI LAENDELEA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA NJIA YA MTANDAO KATIKA KIPINDI HIKI AMBACHO DUNIA INAKABILIWA NA JANGA LA COVID-19.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akichangia mada katika mkutano wa WMO (TCC-1), tarehe 27 Aprili, 2020

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akiwasilisha mada katika mkutano wa WMO (TCC-1), tarehe 28 Aprili, 2020

 Dar -es -Salaam; Tarehe 29 Aprili 2020.

Wakati Dunia inakabiliwa na janga la COVID-19, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa njia ya mtandao. Akizungumzia utendaji wa Shirika hilo Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) amesema uongozi wa WMO umekuwa na vikao vya mara kwa mara kwa njia ya mtandao ambavyo pamoja na mambo mengine umewekwa utaratibu wa kuhakikisha huduma za hali ya hewa duniani zinaendelea kutolewa katika kipindi hiki cha janga la COVID-19.

Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Uratibu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) First Session of the WMO Technical Coordination Committee (TCC-1), ulifanyika kwa njia ya mtandao (Telecoference) kuanzia tarehe 27 hadi 29 Aprili 2020 na Dkt. Agnes Kijazi  alishiriki mkutano huo. Akichangia mada inayohusu Bodi ya Utafiti ya Shirika hilo (WMO Research Board), Dkt. Kijazi aliishauri Bodi hiyo kuhakikisha kwamba mojawapo ya vipaumbele vyake iwe kuzisaidia Nchi Wanachama hususan nchi zinazoendelea katika utafiti wa mifumo mipya inayoibuka siku hizi kutokana na mabadiliko ya tabia nchi (unusual systems) ambayo imeonekana kuleta athari kubwa kwa jamii.

Dkt Kijazi aliongeza kusema kwamba utafiti ni muhimu katika kuboresha huduma za hali ya hewa hata hivyo nchi wanachama wa WMO zina uwezo tofauti wa kufanya utafiti katika masuala ya hali ya hewa, hivyo ni muhimu Bodi ya utafiti ya WMO ikaweka katika vipaumbele vyake namna itakavyosaidia masuala ya utafiti katika ngazi ya nchi na kanda, hususan mambo yanayoibuka kama vile mifumo inayosababisha vipindi vya mvua kubwa, upepo mkali, joto kali, baridi kali, kubadilika kwa misimu ya hali ya hewa, jambo ambalo liliungwa mkono na wajumbe wa mkutano huo.

Awali, akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano huo Dkt. Albert Martis ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa WMO, alitoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19, na kuziomba Taasisi za Hali ya Hewa kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa vile zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi hususan kuchangia katika kuimarisha usalama wa watu na mali zao.

Bodi ya Utafiti ya WMO ni miongoni mwa vyombo vipya (WMO Bodies) vilivyoundwa na Mkutano Mkuu wa 18 wa WMO uliofanyika Juni 2019, ikiwa ni mpango mkakati wa WMO wa mwaka 2020 hadi 2023 wa kuimarisha mchango wa tafiti za hali ya hewa katika kuboresha huduma za hali ya hewa ili zichangie ipasavyo katika maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Bodi hiyo inayoongozwa na Makamuwa Kwanza wa Rais wa WMO iliwasilisha utaratibu wa namna itakavyotekeleza majukumu yake na vipaumbele ilivyojiwekea, ikiwa ni pamoja na kuimarisha masuala ya ubunifu na kufanya tathmini ya athari za ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) katika utoaji wa huduma za hali ya hewa duniani.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, Dkt Kijazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la WMO la kujenga uwezo (Capacity Development Panel), aliwasilisha mada mbili katika kikao hicho kuhusiana na namna jopo hilo litakavyotekeleza majukumu yake (Rule of Procedures) na litakavyoshirikiana na vyombo vingine vya WMO na Taasisi nyingine kote duniani (Coordinated Approach to Capacity Development). Wajumbe walichangia mada hizo na kusisitiza umuhimu wa kuzisaidia nchi wanachama ili kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa maendeleo endelevu. Ilifafanuliwa kwamba jopo hilo la kujenga uwezo ni suala mtambuka katika WMO hivyo liweke vipaombele vyake vitakavyowezesha kuzijengea uwezo sekta mbali mbali hasa katika nchi zinazoendelea.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe takribani 38 kutoka kote Duniani wakiwemo viongozi wote wandamizi wa WMO ikiwa ni pamoja na Rais wa WMO, Prof. Gerhard Adrian (Ujerumani); Makamu wa Kwanza wa Rais, Prof. Celeste Saulo (Argentina); Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Albert Martis (CuraƧao); Makamu wa Tatu wa Rais, Dkt. Agnes Kijazi  (Tanzania); na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas (Finland). Viongozi hao ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Uratibu ya WMO.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...