Thursday, January 28, 2021

WANANCHI WA BAGAMOYO NA TANGA WAFURAHISHWA NA JUHUDI ZA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.






Bagamoyo - Tanga, Tarehe 19 Januari, 2021.

Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania imekutana na wadau kutoka sekta ya uvuvi pamoja na wananchi kwa ujumla ambapo lengo la kukutana na wadau hao ni kutoa uelewa wa taarifa za hali ya hewa pamoja na kuwapa njia mbalimbali ambazo wanaweza kutumia ili kupata kirahisi taarifa za hali ya hewa. Mkutano huo ulifanyika katika Bandari ya Bagamoyo, Bandari Tanga pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzia tarehe 15 mpaka 19 Januari, 2021.

Warsha hiyo iliandaliwa na TMA na kufadhiliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization – WMO), chini ya mwamvuli wa Programu ya kidunia ya kuwaongezea ujuzi waandaaji na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa barani Afrika (Weather and Climate Information Services for Africa - WISER).

 

Washiriki walikumbushwa kuwa Mamlaka ya Hali Ya Hewa inatoa huduma zake kwa ajili ya usalama wa watu na mali zao hivyo kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha kua anafatilia taarifa hizo ili kuepukana na majanga yanayoweza kutokea.

Aidha, wakati wa mkutano huo, mambo mbali mbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na uwelewa wa taarifa za hali ya hewa, uandaaji wa taarifa za hali ya hewa za muda mfupi, wa kati na mrefu, usambazaji wa taarifa za hali ya hewa, uandaaji wa taarifa za hali ya hewa kwenye maeneo madogo na mipaka ya matumizi ya taarifa husika pamoja na kupokea mirejesho ya wadau juu ya matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwenye maeneo.

Kwa upande wa washiriki walishukuru na kufurahishwa sana na Mamlaka kwa juhudi walizozichukua katika kutoa tofauti, pamoja na kuongeza thamani kwa wadau kuweka ushauri na madhara yanayo tarajiwa kwenye taarifa za hali ya hewa zilizo boreshwa. Wakatoa mapendekezo yao kuwa kuwepo na mikutano ya namna iyo mara kwa mara ili wananchi wengi waweze kufikiwa kwa wakati na kuwafikishia taarifa za sahihi.

Monday, January 18, 2021

TMA YAENDELEA KUMILIKI CHETI CHA UBORA WA HUDUMA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA KWA KIPINDI CHA MIAKA KUMI (10) SASA.

 

Dar es salaam,Tarehe 16 Januari, 2021

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kumiliki cheti cha kimataifa cha uthibitisho wa utoaji huduma bora za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga kwa mara nyingine. Mamlaka ambayo imekuwa na cheti hiki kwa miaka kumi sasa, ni miongoni mwa Taasisi chache za hali ya hewa barani Afrika kufanikiwa kushikilia cheti hicho kwa kipindi kirefu.

Mafanikio hayo yamepatikanabaada ya kukamilika kwa ukaguzi uliofanyika kwa njia ya mtandao na Kampuni ya Kimataifa ya Certech kutoka Canada, kuanzia Tarehe 11 hadi 15 Januari 2021 katika vitengo na ofisi mbalimbali ndani ya Mamlaka, Makao Makuu na Mikoani. Ukaguzi huu ulifanyika kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO 9001:2015) na ulimalizika kwa taarifa nzuri ya kwamba TMA imeboresha sana mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo inastahili kuendelea kumiliki cheti hicho cha ubora cha kimataifa.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alisema kuwa Mamlaka imeanza kumiliki cheti hicho cha ubora tangu mwaka 2011, ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho kwa vigezo vya ubora vilivyoainishwa katika mwongozo wa “ISO 9001:2008”, na ilipofika mwaka 2017 Tanzania kupitia TMA ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha inafanikiwa kupata cheti kipya kwa mujibu wa vigezo vipya vya “ISO 9001:2015,” ambacho kiliifanya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa nchi ya tatu barani Afrika ambayo taasisi yake ya hali ya hewa imepata cheti hicho kabla ya Septemba 2018 iliyokuwa ni mwisho wa matumizi ya cheti cha zamani.

“Mamlaka imekuwa ikikaguliwa kimataifa kila mwaka na mkaguzi kutoka nje ya nchi ili kuangalia ubora wa huduma zitolewazo, ni furaha kubwa kuona bado TMA inaendelea kuwa taasisi ya mfano kwa taasisi zingine za hali ya hewa barani Afrika na nje ya Afrika kwa kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa. Mpaka sasa TMA imefanikiwa kutoa mafunzo kwa baadhi ya taasisi za hali ya hewa katika nchi za SADC, EAC na zingine zikiwemo Saudi Arabia, Libya, Nigeria, Maldives, n.k kuhusu jinsi ya kufanikisha upatikanaji wa cheti hiki pamoja na kuboresha weledi wa wataalamu katika Taasisi zao za Hali ya Hewa. Mafanikio haya ni kutokana na ‘team work’ iliyopo baina ya menejimenti na watumishi wa Mamlaka, weledi, bidii na miongozo mizuri tuliyojiwekea ya kuhakikisha tunafanikiwa ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa ukaguzi wa ndani mara kwa mara”. Alisema Dkt. Kijazi.

Aliongeza kwa kusema kwamba upatikanaji wa cheti hicho unaihakikishia dunia kwamba anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa liko salama kwa ndege zote za kimataifa kuruka kwani ilishakubalika kimataifa kwamba kwa nchi ambazo taasisi zao za hali ya hewa hazijapata cheti hicho cha ubora ndege hazitaruka katika anga la nchi hizo. Dkt. Kijazi alisema TMA inajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia sekta ya usafiri wa anga kwani katika viwanja vyote vya ndege nchini huduma za hali ya hewa zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Hata katika viwanja ambavyo ndege hazitui kwa saa 24, TMA inaendelea kupima hali ya hewa katika viwanja hivyo kwa saa 24 ili kukidhi matakwa ya kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Aliwapongeza watumishi wa TMA kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha TMA inatimiza majukumu yake.

Awali wakati akikamilisha ukaguzi huo, mkaguzi wa nje kutoka Certech - Canada Bwana Frank Strohmeier, alisema TMA imekuwa ikiboresha kila mara mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo kwa mwaka huu, hapakuwa na hoja (nonconformity) yoyote ambayo ingehitaji kutolewa maelezo na kupelekea kuhitajika kwa marekebisho katika mfumo wa utoaji huduma. Hivyo maeneo yote ambayo TMA imekaguliwa yamekuwa na ubora wa hali ya juu pasipo kuwa na mapungufu yoyote. Alifurahishwa na jinsi ambavyo ukaguzi umefanyika kwa njia ya mtandao ukiwa na mafanikio makubwa pasipo changamoto yoyote ya teknolojia hivyo akawapongeza sana wataalam wa ICT wa TMA kwa kufanya kazi zao kwa weledi. Alimalizia kwa kuipongeza menejiment nzima ya TMA kwa kazi nzuri inayofanyika.

“Nawapongeza sana kati ya taasisi za hali ya hewa ambazo kampuni yangu imekagua katika nchi mbali mbali duniani sijawahi kuona taasisi ambayo huduma zake zinaendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka kama ilivyo kwa TMA. Mwaka huu sina hoja yoyote mifumo yote imeboreshwa, wafanyakazi wana weledi wa hali ya juu na wanafahamu wanachokifanya, taratibu zote mlizojiwekea mnazitekeleza ikiwemo jinsi ya kutoa utabiri na kuufikisha kwa watumiaji katika sekta ya usafiri wa anga kwa wakati, utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa katika anga, uhakiki wa usahihi wa utabiri unaotolewa katika sekta ya usafiri wa anga, upimaji wa weledi wa watumishi wanaofanyakazi katika viwanja vya ndege, hali ilivyokuwa 2018 sivyo ilivyo 2019 uboreshaji ni wa hali ya juu, nawapongeza sana”. Alisema Bwana Frank kutoka kampuni ya Certech iliyoko nchini Canada.

Friday, January 15, 2021

WITO WATOLEWA VYOMBO VYA HABARI KURUSHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KILA SIKU.



Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi. Godfrey Kasekenya (MB) akizungumza na menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati wa ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 14/01/2021.


Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi akitoa hotuba wakati wa ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 14/01/2021.



Picha mbalimbali wakati wa ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 14/01/2021.


















Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi. Godfrey Kasekenya (MB) (katikati), akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi (kulia, mwenye suti ya blue) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi (wa tatu kushoto) na Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika picha ya pamoja.






Dar es Salaam; Tarehe 14 Januari, 2021;

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi. Godfrey Kasekenya (MB) ametoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha wanawahabarisha wananchi kuhusu taarifa za hali ya hewa ya kila siku ili kuweza kujipanga na kuepukana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa na kusisitiza kuwa hali ya hewa ni kazi ya kisayansi na sio ya kubahatisha.

Hayo yalizungumzwa katika ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 14/01/2021. Lengo la ziara hiyo ni kuifahamu TMA, kazi wanazofanya na kutambua changamoto za kiutendaji ili kuweza kufanya maboresho stahiki. 

“Narudia tena, vyombo vya habari vyote, suala la taarifa za hali ya hewa liwe ni suala la lazima na watoe nafasi kubwa kwaajili ya kuwahabarisha wananchi, kwani kupitia vyombo vya Habari taarifa zitaweza kuwafikia wananchi kwa wakati na kuifanya TMA itekeleze majukumu yake kwa tija. Vinginevyo TMA itakuwa inafanya kazi na taarifa zake hazitumiki na hazisaidii wananchi katika kupunguza athari za majanga kwasababu ya kutokuzifahamu”. Alizungumza Mhe. Kasekenya.

Mhe. Kasekenya aliendelea kwa kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi data za hali ya hewa za muda mrefu katika njia ya kielektroniki ili kuweza kusaidia katika maendeleo ya nchi, huku akitoa mfano wa ujenzi wa madaraja katika maeneo yenye historia ya mvua kubwa kwa kuangalia hali ya hewa ya muda mrefu itakayosaidia kujenga madaraja imara yasiyoathiriwa na mafuriko. Aliendelea kwa kuipongeza TMA kwa kupewa majukumu ya kusaidia nchi zingine katika masuala ya hali ya hewa, hii ni kutokana na uongozi bora wa mkurugenzi mkuu Kitaifa na Kimataifa. Alisema Mhe. Kasekenya.

Mheshimiwa Naibu Waziri aliiagiza TMA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na aliahidi katika utaratibu wa kuboresha maslahi ya watumishi kama alivyoahidi Mhe. Rais watumishi wa TMA watakumbukwa pia. Alisema Taaluma ya hali ya hewa ni kati ya taaluma ambazo ni ‘rare profession’ kwani inachukua muda mrefu kumuandaa mtaalam na mafunzo hayo yanapatikana nje ya nchi ukiacha shahada ya kwanza inayotolewa chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Awali, wakati akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi kupitia taarifa yake fupi aliishukuru Serikali kwa uwekezaji uliofanyika katika sekta ya hali ya hewa na hivyo kuongeza usahihi wa utabiri, na kuiomba Wizara kuwezesha kufanikisha maslahi ya watumishi wa Mamlaka kwa kuwapatia mishahara iliyopendekezwa baada ya zoezi la “job evaluation” ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

“Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi ambazo watumishi wa Mamlaka wanazifanya zinahitaji weledi wa hali ya juu ambapo mishahara wanayopata ni midogo, kazi hizi zinafanyika kwa saa 24 siku 7 kwa wiki bila kujali jua, mvua, upepo mkali, wanyama wakali, nyoka n.k, watumishi hutoka nje kupima taarifa za hali ya hewa kila nusu saa kwa vituo vyote vilivyopo maeneo mbalimbali nchini”. Alifafanua Dkt. Nyenzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru Mhe. Kasekenya kwa kutembelea TMA na kuahidi kuisaidia Mamlaka kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuendelea kuboresha mtandao wa vituo vya hali ya hewa na maslahi ya watumishi. Dkt. Kijazi aliamuahidi Mhe. Waziri kwamba maagizo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo TMA itayatekeleza.

Aidha, aliendelea kwa kufafananua kuwa TMA imeshaanza kazi ya kuzihifadhi data za hali ya hewa katika mfumo wa kidigitali na kuahidi kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa weledi, kwa upande wa ushirikiano na vyombo vya habari, Dkt. Kijazi alisema, hivi sasa Mamlaka inaushirikiano mzuri na mpaka sasa zaidi radio za kijamii 50 zinasambaza utabiri wa hali ya hewa unatolewa kila siku na hivyo kusaidia kuwa daraja la TMA na jamii. Vilevile, alitoa ufafanuzi kuhusu kuonekana kwa miji mingine katika vyombo vya habari vya kimataifa na miji ya Tanzania kutokuonekana, akisema ni utaratibu ambao upo ila suala hilo litafanyiwa kazi ili kuwekwa sawa.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...