Monday, May 15, 2023

TANZANIA YAPEWA KIPAUMBELE UBORESHAJI WA MIUNDO MBINU YA HALI YA HEWA

Mwakilishi Mkazi Tanzania, Mpango wa Umoja wa Mataifa Kusaidia Maendeleo Duniani (UNDP), Bi. Christiane Musisi, akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundo mbinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.


Mwakilishi kutoka Taasisi ya Hali ya Hewa Denmark (DMI), Bw. Christian Johansen akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundombinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.


Baadhi ya washiriki wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundombinu ya hali ya hewa nchini.






Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya nchi katika miundo mbinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.




Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark, zimekutana na wadau katika warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya nchi katika miundo mbinu ya hali ya hewa ili kuweza kufanya maboresho ambayo yatasaidia kuleta tija katika utoaji huduma za hali ya hewa kwa maendeleo ya Taifa.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa Tanzania imepata fursa ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 26 duniani ambazo zimepewa kipaumbele katika kuimarisha huduma za hali ya hewa kupitia miundo mbinu ya uangazi wa hali ya hewa chini ya mwamvuli wa Mfuko wa Kuimarisha Uangazi wa hali ya hewa (Systematic Observations Financing facility-SOFF). Mfuko huu umekuwa ukichangiwa nan chi mbalimbali duniani, na wadau mbalimbali wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Mpango wa Umoja wa Matatifa wa Kusaidia Maendeleo Duniani (UNDP).

 

Dkt. Chang’a alisema, ‘fursa hii ni muhimu kwa Tanzania hususani kipindi hiki ambacho dunia ikiwemo nchi yetu inakabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, changamoto hizi zinahitaji msukumo wa kipekee katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa lakini vilevile, utoaji wa huduma hususan huduma za utabiri na tahadhari za hali mbaya ya hewa ”. Alisema Dkt. Chang’a. 

 

“Hii ni mojawapo ya jitihada ambazo zinaenda kuchangia katika jitihada kubwa zinazofanywa na serikali yetu ya kuimarisha huduma za hali ya hewa  na kuongeza uwezo wetu wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Tunaishukuru sana Serikali”. Aliongeza Dkt. Chang’a.

 

Kwa upande wake Bw. Christian Johansen, mwakilishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI),alisema ushirikiano baina ya Tanzania na Denmark ni wa muda mrefu na unaendelea kukua. Ushirikiano wa sasa baina ya TMA, DMI na UNDP unalenga kuboresha huduma za hali ya hewa kwa kuimarisha miundombinu ya uangazi pamoja na kuendeleza  mahusiano mazuri yaliyoweka baina ya nchi hizi mbili. Alisema kupitia program ya SOFF waliweza kutembelea katika maeneo ya Singida, Dodoma, Shinyanga, Mwanza na Tabora, na kufanya tathmini ya uwezo na mahitaji katika kuimarisha uangazi, na kupitia warsha hii wanatarajia kupata taarifa zaidi za maeneo mengine ya nchi yanayohitaji maboresho na uimarishaji wa mfumo wa uangazi.

 

Naye mwakalishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Bi. Christine Musisi alishukuru kwa mahusiano mazuri baina ya UNDP na TMA, ikiwemo misaada mbalimbali ambayo UNDP imekuwa ikitoa kusaidia uimarishwaji wa huduma za hali ya hewa. Alieleza kuwa takwimu zinaonesha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo matukio ya mafuriko, na hivyo programu hii itasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa na za uhakika na hivyo kuchangia katika kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta muhimu kama vile kilimo, mifugo, nishati, uchukuzi, afya na maji. Aidha, aliongeza kusema kuwa uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa ni kwa manufaa ya nchi na dunia kwa ujumla.


 

Monday, May 8, 2023

ELIMU YA HALI YA HEWA YATOLEWA KWA WATU WENYE UHITAJI MAALUM





















Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA) imewajengea uwezo watu wenye uhitaji maalumu kwa kutoka elimu ya masuala mbalimbali ya Hali ya Hewa ikiwemo uchambuzi wa hali ya hewa kuanzia ngazi ya uangazi hadi usambazaji, Elimu hii pia ilihusisha aina mbalimbali za utabiri wa hali ya hewa kuanzia utabiri wa muda mfupi, kati, mwezi, msimu, hali mbaya ya hewa na athari zake, mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi pamoja na majukumu ya Mamlaka, kupitia warsha iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC), Ikwiriri, Rufiji.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Katibu wa SHIVYAWATA Rufiji Bwana Abdul Warusimbi aliishukuru TMA kwa kufika Ikwiriri na kuweza kutoa elimu ambayo itawasaidia katika kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kwa washiriki 100 kutoka Rufiji, Nyamisati na Visiwa vya Chole  na Mafia.

“Katika siku za hivi karibuni kumetokea majanga mbalimbali ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya hali mbaya ya hewa, majanga hayo yamekuwa yakiwaathiri watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa hususani watu wa vijijini.Kupitia TMA wamejifunza kuwa kila hatua ya maisha wanayopiga wanahitaji usaidizi wa  utabiri wa hali ya hewa”Alisema Abdul Warusimbi. 

Kwa upande wake, Bwana. Haji Omari Mpili maarufu kama Mzee Mpili, alisema TMA ina wataalamu waliobobea katika masuala ya hali ya hewa na kuwataka wananchi wa Kusini kuacha kutumia utabiri wa kizamani wa kusoma nyota na kujikita katika utabiri wa kisayansi ambao unafanyiwa utafiti wa kitaalamu. 

“Mfano hivi sasa msimu wa mvua unaisha lakini kuna watu wengine wanaendelea kupanda. Je, mimea hiyo itafanikiwa? taarifa za hali ya hewa kutoka TMA zinaeleza mvua itaanza kipindi gani na itamalizika kipindi gani, ni vizuri kufuatilia taarifa hizo zenye uhakika”. Alisema Mzee Mpili. 

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Bwana. Hassan Said Bakari, Mkuu wa Kituo cha Hali ya Hewa Kilwa Masoko, alisema utabiri wa msimu wa mvua ulitabiriwa kuwa chini ya wastani kwa maeneo ya Kusini mwa nchi na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

“Mamlaka imepokea maoni mbalimbali yaliyotolewa na watu wenye uhitaji maalumu na kupitia maoni yao, TMA itayafanyia kazi ili kuhakikisha  kundi hili maalum linafikiwa kwa urahisi, vilevile Mamlaka imeendelea kuwakumbuhsha kufuatilia taarifa za hali ya hewa zionazotolewa mara kwa mara ili kuweza kufanya uzalishaji wenye tija hususan kipindi hiki cha changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi”.Alisema Bw. Bakari

Bi. Lulu Salimu, mkazi na mkulima kutoka Ikwiriri alieleza namna ambavyo alitumia taarifa za hali ya hewa zilizitolewa mwezi Oktoba 2023 na kufanya maamuzi ya kutumia mbegu za muda mfupi, hivyo kufanikiwa kupata mavuno mengi wakati wakulima wengine wakipata hasara kutokana na kutumia mbegu za muda mrefu.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...