Saturday, October 29, 2022

MWENYEKITI WA BODI TMA APONGEZA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA BARAZA LA WAFANYAKAZI





























Kibaha, Pwani; Tarehe 29 Oktoba, 2022;

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi ameipongeza TMA kwa kutekeleza Mkataba wa Baraza kwa kuhakikisha wajumbe wa Baraza wanakutana mara mbili kwa mwaka. Alieleza hayo wakati akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa TMA la pili kwa mwaka 2022 katika Ukumbi wa Manesi na Wakunga,Kibaha, Pwani, tarehe 29/10/2022.

“Kupitia taarifa ya Mwenyekiti wa Baraza, nimeelezwa kuwa hiki ni kikao cha pili, hivyo naipongeza Mamlaka kwa kuwa na mabaraza mawili kwa mwaka kulingana na Mkataba. Aidha, niendelee kuwapongeza kwa uwakilishi mzuri kwa kuwa na wajumbe tisini na nane kutoka maeneo mbalimbali nchini”. Alisema Dkt. Nyenzi.

Dkt. Nyenzi aliendelea kwa kuipongeza Mamlaka kwa utekelezaji mzuri wa miradi mikubwa na mafanikio yaliyopatikana hususani fanikio la kuboresha miundo mbinu ya hali ya hewa sambamba na kutekeleza agizo la Serikali la kuhamia Dodoma, Makao Makuu ya nchi. Vilevile, aliishukuru Bodi kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Taasisi uliochangia mafanikio hayo.

“Nitumie fursa hii kuwashuruku wajumbe wa Bodi ambao nimefanya nao kazi kwa kipindi cha miaka mitatu kwa utumishi wao uliotukuka uliopelekea mafanikio yote haya yaliyoainishwa na Mwenyekiti wa Baraza hili, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi”. Alieleza Dkt. Nyenzi. 

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi Dkt. Ladislaus Chang’a, akisoma taarifa ya Mwenyekiti wa Baraza kwa niaba ya Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alishukuru Serikali kupitia Wizara na Bodi ya TMA kwa ushirikiano na kazi kubwa iliyofanyika ya kufanikisha malengo ya Taasisi, ambapo viwango vya usahihi wa utabiri vimeendelea kuongezeka, nakutoa wito kwa watanzania kutumia taarifa hizo za hali ya hewa. 

Katika taarifa hiyo, Dkt. Kijazi aliendelea kueleza kuwa “Dhumuni kuu la Baraza hili ni kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ambao utasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi”.

Akielezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Baraza lililopita na Baraza la sasa, Mwenyekiti wa Baraza alisema mafanikio hayo  ni pamoja na “ufanisi wa utekelezaji wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na Kanuni zake, ununuzi wa rada na miundo mbinu kwa ujumla, uboreshaji wa maslahi ya wafanyaki kwa kuendelea kupandishwa vyeo,kubadilishwa kada,ongezeko la mishahara na kuhuishwa kwa miundo ya kada kwa watumishi kufuatia mabadiliko ya Miundo ya Maendeleo ya Watumishi”.







Wednesday, October 26, 2022

MVUA ZA MSIMU: SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUJIPANGA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MVUA UNAOTARAJIWA KUTOKEA.

 

 



Dar es Salaam, Tarehe 26/10/2022

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo yakijumuisha mikoa ya (Tabora, Kigoma Kusini, Katavi, Mbeya, Rukwa, Soingwe,Njombe, Iringa, Ruvuma na Morogoro Kusini) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023.

Wakati akitoa utabiri huo kwa niaba ya Mkurugenzi Wakati wa akitoa utabiri huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, TMA alisema katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza, hivyo sekta mbalimbali zinatakiwa kujipanga na kukabiliana na hali hiyo. 

“Upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za Msimu na kuathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo. Vilevile, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali kama vile umwagiliaji na uzalishaji wa nishati. Mamlaka zinashauriwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu”. Alifafanua Dkt. Kabelwa. 

Alisema, “Katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hata hivyo, ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari- Aprili, 2023). Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo mengi.Maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma mvua za Msimu  zinatarajiwa kuanza  kwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023“.Alizungumza Dkt. Kabelwa

Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara.  Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Akizingumzia kuhusu Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2022 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, alisema Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba), msimu unatarajiwa kuendelea kama utabiri ulivyotolewa tarehe 2 Septemba, 2022, ambapo maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani. Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari, 2023.

Kwa maelezo kamili kuhusu utabiri huu tembelea http://www.meteo.go.tz/

Tuesday, October 25, 2022

WASHINDI WA TUZO YA MWAHABARI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA 2022 WAPONGEZWA

 





















Dar es Salaam; Tarehe 25 Oktoba, 2022;

"Natoa pongezi zangu za kipekee kwa washindi wa Tuzo ya mwanahabari bora wa mwaka wa habari za hali ya hewa Tanzania 2022 pamoja na kuwapa hamasa wanahabari wengine kuendelea kufanya kazi bora zaidi na kuziwasilisha taarifa hizo ili ziweze kutambuliwa na Mamlaka na kuwa sehemu ya  mchakato wa Tuzo hii katika wakati ujao”. Alizungumza hayo Dkt. Nyenzi wakati akifungua hafla ya utoaji tuzo ya mwanahabari bora wa mwaka wa habari za Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), 2022 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano katika hoteli ya Tiffany Diamonds, Dar es Salaam, Tarehe 25 Oktoba 2022.

Dkt. Nyenzi alianza kwa kukabidhi Tuzo hizo za Mwanahabari bora, ambapo mshindi aliyepewa tuzo ya jumla alikuwa ni Irene Mark kutoka gazeti la Jamvi la habari na blog ya habari mseto, mshindi wa upande wa magazetini alikuwa Irene Mark kutoka gazeti la Jamvi la habari, mshindi wa upande wa Luninga na redio alikuwa Mussa Kharid kutoka Kiss FM, na mshindi wa upande wa mitandao ya kijamii alikuwa Noel Lukanuga kutoka Uhondo TV.

Aidha, Dkt. Nyenzi aliongezea kwa kuwapongeza wanahabari na vyombo vyote vya habari kwa kuendelea kushirikiana na TMA katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii pamoja na kuipongeza TMA kwa kuendeleza ushirikiano huo uliosababisha jamii kupata taarifa kwa wakati na kujilinda au kupunguza athari mbaya za hali ya hewa sambamba na kuijengea jamii uwezo wa kutumia taarifa hizo kwa maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Ndugu Mbaraka Islam nguli wa habari hapa nchini ambaye ni mhariri gazeti la Raia Mwema  aliwakumbusha wanahabari kufuata vigezo vilivyoainishwa na Mamlaka na kuwa wabunifu pale wanapopata taarifa kutoka TMA kwa kuhusisha taarifa hizo na shughuli za kijamii kutoka sekta mbalimbali ili taarifa zao ziwe na tija kwa jamii.

Kabla ya hafla hiyo ya Tuzo kwa wanahabari bora, Mamlaka ilipata muda wa kujadiliana na wanahabari kupitia warsha ya wanahabari iliyofanyika hotelini hapo kwa lengo la kutoa uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 unaotarajiwa kutolewa rasmi katika ukumbi wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo plaza tarehe 26 Oktoba 2022.

Kupitia warsha hiyo yenye kauli mbiu “Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”, wanahabari wametakiwa kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na kutafuta, kupata na kuwasilisha ufafanuzi na maelezo ya ziada ya kisekta kutoka kwa wataalam ili taarifa sahihi ziweze kufikia jamii kwa ukamilifu

Aidha, wanahabari wamekumbushwa kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa TMA kuelezea na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zao za kila siku

Monday, October 24, 2022

DKT. NYENZI: TAARIFA ZA HALI YA HEWA NI CHACHU YA KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA.

 














Dar es Salaam; Tarehe 24 Oktoba, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili utabiri wa mvua za msimu unaotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni Tabora, KigomaKusini,Katavi,Mbeya,Rukwa,Songwe,Njombe,Iringa,Ruvuma,Mtwara,Lindi,Dodoma, singida na Morogoro Kusini . Katika ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotels uliopo jijini Dar es Salam, Tarehe 24 Oktoba 2022, mgeni rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi amehimiza wadau kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa ambazo ni chachu katika kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini.

“Taarifa za hali ya hewa zinalenga katika kusaidia nchi kufikia malengo ya mpango wa Taifa katika kujenga uchumi wa viwanda kwa kusaidia kupunguza athari zitokanazo na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa ili kusaidia kulinda mafanikio ya uwekezaji katika miundo mbinu ya uchukuzi ikiwemo barabara, reli na vyombo vya usafiri majini”. Alisema Dkt.Nyenzi

Dkt. Nyenzi aliongezea kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kuendelea kuijengea uwezo TMA, hatua ambayo imeisaidia kuboresha utabiri wa hali ya hewa na kusaidia Taifa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo upungufu wa mvua, mafuriko, joto na baridi kali  pale zitakapojitokeza.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi ameelezea namna serikali ilivyoendelea kuijengea uwezo Mamlaka kwa kuboresha miundo mbinu yake ambayo kwa njia moja au nyingine inasaidia kukuza uchumi wa nchi.

Dkt. Kijazi amesema mtandao wa rada upo katika hatua za mwisho ili kukamilika, huku vituo vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe vikizidi kuongezwa na mbiundombinu ya uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ikiendelea kuboreshwa, Aidha mitambo ya mawasiliano imeendelea kuboreshwa ili taarifa hizi ziweze kuwafikia wadau kwa wakati, na pia wataalam wameendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo mbalimbali na hivyo kuwapa uwezo wa kufungasha taarifa zilizoboreshwa.

Aidha, Dkt. Kijazi aliwashukuru ILRI kutoka  Nairobi ambao wamefadhili kwa sehemu kikao hicho cha wadau.

Aidha, wadau mbalimbali wa hali ya hewa walielezea namna wanavyozitumia taarifa za hali ya hewa katika kujiandaa na kukabiliana na hali ya hewa tarajiwa katika sekta zao, ambapo mdau kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ndugu Emmanuel Kato (Afisa Malisho), alielezea namna sekta hiyo inavyojiandaa katika kukabiliana na hali ya hewa tarajiwa na maandalizi hayo ni pamoja na kuchimba visima virefu vya maji na ujenzi wa mabwawa katika kupunguza au kuepusha migogoro ya wafugaji katika kutafuta maji kwaajili  ya  mifugo pale upungufu wa mvua unapojitokeza.

Kwa upande wa mdau wa kilimo Juma Makandi, alisema kupitia taarifa za TMA timu ya wataalam imeweza kutembelea maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula na kwa sasa inaendelea na tathmini na ripoti itatolewa baada ya kazi kukamilika, naye, mdau wa kutoka TANESCO James Kirahuka alisema umuhimu wa taarifa za hali ya hewa katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini ni pamoja na kusaidia katika kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme kama vile kuanguka kwa nguzo za umeme.


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...