Wakati Mheshimiwa
Rais John Pombe Magufuli akielekea kupokea Uenyekiti wa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania kupitia Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi amekabidhiwa Uenyekiti
wa Kamati ndogo ya Sekta ya Hali ya Hewa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) “SADC Sub-Sectoral Committee on
Meteorology (SADC SCOM) kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, Tanzania
kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi amechaguliwa
bila kupingwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi
za SADC “SADC Meteorological Association of Southern Africa (SADC-MASA)” kwa
kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2019. Bwana Wilbert Timiza Muruke ambaye amemwakilisha Dkt. Kijazi amekabidhiwa
nafasi hizo katika Mikutano ya SADC-SCOM na SADC-MASA iliyofanyika kwa
kufuatana Jijini Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 5 hadi 9 Agosti, 2019.
Kama ilivyo kawaida
baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kukabidhiwa Uenyekiti wa
SADC, Sekta zingine zote zinakuwa chini ya uenyekiti wa Tanzania, hivyo kwa
upande wa Sekta ya Hali ya Hewa, tayari TMA imekwishakabidhiwa Uenyekiti wa
kamati hiyo ya SADC Sekta ya hali ya hewa (SADC SCOM) kutoka kwa Taasisi ya Hali
ya Hewa ya Namibia. Aidha, Uenyekiti wa Tanzania kuongoza umoja wa Taasisi za
Hali ya Hewa za SADC (SADC MASA) utadumu kwa miaka miwili, ambapo Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya hali ya hewa ya Lesotho amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC
MASA. Kabla ya kupokea nafasi hiyo ya kuwa Mwenyekiti wa MASA, Dkt. Kijazi
alikuwa Makamu mwenyekiti na Bwana Franz Uirab kutoka Namibia alikuwa
Mwenyekiti.
Akipokea dhamana
hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Meneja wa Mahusiano ya Hali ya Hewa
Kimataifa, Ndugu Wilbert Timiza Muruke ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu
katika Mikutano hiyo, alishukuru kwa nafasi hizo na kumpongeza aliyekuwa
Mwenyekiti wa SADC SCOM na SADC MASA ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Hali
ya Hewa ya Namibia, Bwana Franz Uirab kwa mafanikio yaliyopatikana katika
kipindi cha uongozi wake. Ndugu Muruke kwa niaba ya Mwenyekiti, Dkt. Kijazi aliahidi
kutoa na kuomba ushirikiano wa taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wa
SADC, ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kutekeleza malengo yaliyowekwa
ya kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa, ziweze kuchangia ipasavyo katika
uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika ukanda
wa SADC. Hii ikiwa pia ni dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kuelekea kupokea uenyekiti wa SADC ya kuleta mapinduzi ya viwanda na ubunifu
hasa kwa kuwalenga vijana katika nchi Wanachama wa SADC.
Mikutano hii
imefanyika kulingana na ratiba ya mikutano na vikao vya kisekta ya SADC, na
imejadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa sekta ya hali ya hewa katika
eneo la SADC pamoja na kupitia hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa Mawaziri
uliopita. Aidha mapendekezo mapya yatakayowasilishwa katika mkutano ujao wa Mawaziri
wenye dhamana na sekta za uchukuzi, TEHAMA na hali ya hewa utakaofanyika mwezi
Septemba Jijini Dar es Salaam yametolewa. Mapendekezo haya ni pamoja na
kuwahimiza nchi wanachama wa SADC kuendelea kuboresha miundombinu ya upimaji wa
hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kutekeleza mkataba wa Minamata ambao unahitaji
nchi wanachama kuondokana na matumizi ya zebaki katika sekta mbalimbali, Nchi
wanachama kuhakikisha wanaendelea kuboresha huduma na kupata cheti cha ubora
cha kimataifa na kukitunza hususan katika utoaji wa huduma za hali ya hewa
zitolewazo kwa usafiri wa anga (ISO 9001: 2015). Tanzania kupitia TMA tayari
imeshapata cheti hicho mwaka 2017. Katika Mikutano hii miwili Tanzania
imewakilishwa na Bwana Wilbert Timiza Muruke, Mtaalamu Mwandamizi wa hali ya
hewa na Meneja wa Mahusiano ya Hali ya
Hewa Kimataifa (aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu) na Ndugu Mathew Ndaki,
Mtaalamu wa hali ya hewa na afisa katika Ofisi ya Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa
ya TMA.
No comments:
Post a Comment