Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza katika mkutano huo unaofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam leo. |
Meza Kuu |
‘Tarehe 26/08/2019: Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Mhandisi Isaack Kamwelwe amehimiza wanasayansi na wataalam wa sekta mbalimbali kuhakikisha wanafanikisha upatikanaji wa mipango madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa 53 wa utoaji wa utabiri wa Hali ya Hewa wa Msimu wa Mvua za Vuli 2019 "Fifty Third Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum" (GHACOF 53) unaofanyika katika Hotel ya Kilimanjaro (Hyatt Regency) kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2019 Dar es Salaam.
'Naamini
baada ya mkutano huu wataalamu mliopo kwenye mkutano huu mtakuja na mpango
madhubuti wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kuweza kupunguza
athari zitokanazo na mabadiliko hayo’, alizungumza Mhe.
Kamwelwe.
Aidha, Mheshimiwa Kamwele aliwakumbusha
wataalam hao kutoka nchi kumi na moja za pembe ya Afrika umuhimu wa kuhusisha
utabiri wa jadi (Indigenous knowledge) katika kuboresha utabiri. Alisema kuna
wadudu ambao wakionekana inaashiria kuanza kwa mvua na kuna ambao wakionekana inaashiria
mvua si za kuridhisha, aliwataka wanasayansi hao kufanya uchambuzi wa kina.
Sambamba na maelekezo hayo, Mheshimiwa
Kamwele aliwakaribisha washiriki wa kongamano hilo kutembelea sehemu za vivutio
vya utalii vilivyopo hapa nchini na aliwataka kujifunza maneno machache ya
Kiswahili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la
Hali ya Hewa Duniani, Dkt.Agnes Kijazi alimweleza mhe. Waziri kuwa kupitia
mikutano hiyo kumekuwa na maboresho makubwa kwenye mfumo wa mawasiliano kati ya
wanasayansi na wataalamu kutoka sekta mbalimbali hivyo kusaidia matumizi sahihi
ya taarifa za hali ya hewa zitolewazo na taasisi za hali ya hewa za nchi za
Pembe ya Afrika.
Pia, Dkt. Kijazi aliishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais John Joseph Pombe
Magufuli kwa kutoa kipaombele katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini.
Aliendelea kwa kusema kuwa uwekezaji
unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya hali ya hewa ukiwemo mtandao wa
rada za hali ya hewa ni kielelezo tosha cha umakini wa serikali kuboresha sekta
ya hali ya hewa ambayo ni ya muhimu sana katika kufikia maendeleo endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa taasis
za hali ya hewa katika nchi za pembe ya Afrika Dkt. Kijazi aliziomba serikali
za nchi hizo kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na pia aliwashukuru
ICPAC kwa kuendelea kuendesha makongamano hayo ambayo alisema yameendelea kuwa
chachu ya uboreshaji wa utabiri wa msimu katika nchi za pembe ya Afrika.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Taasis
inayosimamia Masuala ya Hali ya Hewa kwa Nchi za Pembe ya Afrika
(IGAD
Climate Prediction and Application Centre (ICPAC)) Dkt. Guleid Artan alielezea lengo
la kongamano hilo kuwa ni
kujadili na kuandaa kwa pamoja utabiri wa msimu wa mvua za vuli za mwezi Oktoba
hadi Desemba 2019, pamoja na kuandaa mikakati ya kukubaliana na hali mbaya ya
hewa kwa msimu huo kwa kulenga sekta muhimu za kijamii na kiuchumi ambazo ni
pamoja na afya, kilimo na usalama wa chakula, maji, nishati n.k.
Mwakilishi
wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Afiesimama aliwajulisha washiriki wa
kongamano hilo kwamba katika mkutano wa WMO Congress uliomalizika hivi karibuni
Afrika ilifanikiwa kuwa na mwakilishi katika ngazi za juu za uongozi wa Shirika
hilo kupitia Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania ambaye alichaguliwa katika nafasi ya Makamu wa tatu wa Rais wa WMO.
Aidha, aliahidi kwamba WMO itaendelea kuzisaidia nchi wanachama kuboresha
huduma zikiwemo nchi za pembe ya Afrika.
Wengine
waliozungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo ni mwakilishi wa Bank ya
maendeleo ya Afrika Dkt. Solomon Ngoze ambae alielezea misaada mbali mbali
iliyotolewa na Bank hiyo katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwenye nchi za
pembe ya Afrika. Mwakilishi wa programu ya WISER Mr. Adam Curtis alielezea
mafanikio yaliyofikiwa katika kutekeleza programu hiyo. Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Buruhani Nyenzi aliwakumbusha washiriki
hao kwamba kongamano la kwanza lilifanyika nchini Zimbabwe mwaka 1996 ambapo
yeye binafsi alikuwa kiongozi wa taasisi iliyohusika na ukame kusini mwa Afrika
ambayo ndiyo iliendesha kongamano hilo. Alionyesha furaha yake kuona kwamba
makongamano hayo yanaendelea kwa ufanisi mkubwa.
GHACOF ni Mkutano
unaojumuisha nchi za Pembe ya Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Somalia,
Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Uganda, Burundi, Rwanda, Djibouti na Eritrea
pamoja na mashirika ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Hali ya Hewa Duniani
(WMO).
No comments:
Post a Comment