Saturday, April 24, 2021

MWENENDO WA KIMBUNGA JOBO KATIKA PWANI YA TANZANIA

 


Dar es Salaam, 24 Aprili 2021 asubuhi:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi. Kimbunga “Jobo” kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia. Kimbunga hicho kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani. Hivyo, “Jobo” kwa sasa ni kimbunga hafifu kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini.

Hata hivyo, kimbunga hafifu “Jobo” kinatarajiwa kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo tarehe 24 na kesho 25 mwezi Aprili, 2021. Izingatiwe kuwa uwepo wa kimbunga hafifu baharini, unatarajiwa kusababisha mawimbi makubwa.

Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...