Dar es Salaam; Tarehe 01 Aprili, 2021.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Nala mkoani Dodoma na Maretoni, Arumeru mpakani mwa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha.
Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mkataba huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alisema kuwa ununuzi wa Rada hizo mbili za mwisho unakamilisha mtandao wa Rada saba nchini.
“Ununuzi wa Rada hizi mbili kwa ajili ya Dodoma na Kilimanjaro unagharimu kiasi cha dola za kimarekani 4,990,447.00, utengenezaji na ufungaji wake utachukua miezi kumi na nne hadi kukamilika kwake”. Alisema Dkt. Nyenzi. Awali Mwenyekiti huyo wa Bodi, aliwataka washiriki wa hafla hiyo fupi kusimama na kuwa na dakika moja ya utulivu ili kumkumbuka Rais wetu Mpendwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye katika kipindi cha uongozi wake huduma za hali ya hewa nchini zimeboreshwa kawa kasi kubwa.
“Rada hizi zinauwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250. Aidha, mitambo hii pia inasaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga letu la Tanzania”. Aliongeza kusema Dkt. Nyenzi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuiwezesha TMA kutengewa fedha za miradi ya maendeleo ambazo zimefanikisha upatikanaji wa Rada 5.
“Katika kipindi kifupi cha miaka mitano ya uongozi wa Jemadari wetu Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, TMA imeweza kutimiza lengo la kuwa na Rada saba (7) za hali ya hewa nchini, haya ni mafanikio makubwa sana kwa Mamlaka kuweza kupatikana kwa Rada hizo kwa kipindi kifupi”. Alizungumza Dkt. Kijazi.
Aidha, Dkt. Kijazi aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ili kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinatolewa kwa viwango vya kimataifa na hivyo kuweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu. “Mabadiliko ya hali ya hewa (Climate change) yamekuwa na athari kubwa duniani kote, ambapo hapa nchini tumeshuhudia kubadilika kwa mifumo ya hali ya hewa yenye athari katika utabiri wa msimu na matukio ya majanga yanayosababishwa na hali mabaya ya hewa, ambapo kuwepo kwa vifaa vya kisasa ukiwepo mtandao wa rada kutaiwezesha TMA kutoa huduma bora kwa maendeleo ya Taifa letu”. Alisistiza Dkt. Kijazi.
Naye, mwakilishi kutoka Kampuni ya Enterprise Electronics Corporation (EEC) kutoka Marekani, Bw. Edwin Kisanga alisema mkataba huo unajumuisha pia mafunzo ya wataalamu kutoka TMA yatakayofanyika hapa nchini na kiwandani kule Marekani.
Mkataba huo umesainiwa baina ya TMA na EEC, ukishuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt Buruhani Nyenzi, Mjumbe wa Bodi ya TMA kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka, Mwanasheria kutoka TMA Adv. Emanuel Ntenga, Mwanasheria kutoka EEC Adv. Seni Malimi, menejimenti ya TMA na baadhi ya wageni waalikwa.
No comments:
Post a Comment