Dar es Salaam, 22 Aprili 2021:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Kimbunga Jobo kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya nchi yetu ambapo leo usiku wa kuamkia tarehe 23/4/2021 kimbunga hiki kinatarajiwa kuwa umbali wa takriban kilomita 410 kutoka pwani ya mkoa wa Lindi. Hata hivyo, kimbunga Jobo kinatarajiwa kupungua nguvu yake kadri kinavyosogea katika pwani ya Tanzania.
Aidha, izingatiwe kuwa uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya ongezeko la mvua na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa Pwani.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment