Dar es Salaam, 24 Aprili 2021 mchana:
Taarifa hii inahuisha taarifa ya kimbunga “Jobo” iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania leo asubuhi tarehe 24/04/2021. Mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi unaonyesha kuwa kitovu cha kimbunga hicho kipo umbali wa kilomita 76 mashariki mwa kisiwa cha Mafia.
Kimbunga “Jobo” kwa sasa kinasafiri kwa kasi ya kilometa 20 kwa saa baharini ambayo ni kasi kubwa kwa mwenendo wa vimbunga. Kutokana na kasi hiyo kubwa, kisiwa cha Mafia na maeneo jirani yanatarajiwa kuanza kupata mvua kubwa mapema zaidi leo jioni tarehe 24/04/2021.
Kwa upande mwingine, kuanzia usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 25/04/2021, maeneo ya kusini mwa mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam yanatarajiwa kupata mvua kubwa wakati maeneo mengine ya Lindi, Mtwara na kisiwa cha Unguja pia yanatarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa siku ya kesho Jumapili tarehe 25/04/2021 kwa baadhi ya maeneo. Aidha, pamoja na upepo wa kimbunga kupungua kwa kiasi kikubwa, vipindi vya upepo mkali vinaweza kujitokeza hususan wakati wa mvua kubwa.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza. Izingatiwe kuwa vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko.
No comments:
Post a Comment