Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Wizarani na TMA, Ofisi za wizara, Dar es Salaam |
Ujumbe kutoka TMA (juu) na Ujumbe kutoka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (chini) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mhe. Prof Kabudi, Ofisi za wizara, Dar es Salaam |
‘Nakuahidi
kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wote katika kutekeleza majukumu yako ndani
ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)’. Alisema Mhe. Prof. Palamagamba
Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati
alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt.
Agnes Kijazi.
Katika
mazungumzo hayo, Prof. Kabudi alisema Dkt. Kijazi amekuwa mfano kwa Tanzania na
Afrika hususani kwa wanawake na kuahidi kutoa ushirikiano wenye lengo la
kuhakikisha anafanikisha utekelezaji wa majukumu yake katika nafasi ya Makamu
wa Tatu wa Rais wa WMO na hivyo kuiwakilisha nchi vyema.
Mhe. Prof
Kabudi aliendelea kuelezea umuhimu wa kujiendeleza kielimu kwa watumishi wote
wa Serikali ili kuweza kujijengea uwezo wa kupambana na watumishi au wagombea
wengine kutoka mataifa mbalimbali hususan mataifa yaliyoendelea kwenye nafasi
za juu za kidunia.
Aidha, Mhe.
Waziri alimtaka Mkurugenzi wa TMA kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa
nchini kwa vile ni huduma muhimu sana kwa sekta zingine kama kilimo, uvuvi,
mipango n.k, akitolea mfano wa kazi nzuri iliyofanyika ya kutoa tahadhari za
mara kwa mara za mvua kubwa na kimbunga Kenneth ambazo zilisaidia Serikali
kuchukua hatua stahiki
Naye, Dkt.
Kijazi aliishukuru Wizara kwa namna walivyofanikisha mchakato mzima wa uchaguzi
hadi kupatikana kwa nafasi ya umakamu wa Tatu wa Rais wa WMO na aliahidi
kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania vizuri, kwavile ameona jinsi diplomasia
ya Tanzania inavyokubalika kimataifa.
‘Kwa vile moja
ya jukumu langu kubwa nililopatiwa kusimamia ni eneo la kujengeana uwezo
(capacity building), nitahakikisha mawazo ya nchi zinazoendelea ikiwemo
Tanzania yanawasilishwa na kufanyiwa kazi kwa maendeleo ya sayansi ya hali ya
hewa na hivyo kuboresha huduma za hali ya hewa’. Alizungumza Dkt. Kijazi
Aidha,
aliishukuru Serikali, kupitia Wizira wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa kumuani na kukubali kujitosa katika kinyanga’nyiro hicho. Aliiomba
Serikali iendelee kufanya hivyo kwa wengine ili kukuza diplomasia ya Tanzania
duniani.
IMEANDALIWA NA;
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)
No comments:
Post a Comment