Thursday, July 18, 2019

WATUMIAJI WA ZIWA VIKTORIA KUNUFAIKA NA UBORESHAJI WA UTOAJI WA TAHADHARI ZA HALI MBAYA YA HEWA





Tarehe 18/07/2019. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mpango maalumu wenye lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Viktoria. Mpango huo ulibainishwa wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa ‘HIGH impact Weather lAke sYstem (HIGHWAY)’ uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Ubungo Plaza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a .
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imedhamiria kuongeza ufanisi wa uandaaji na usambazaji kwa wakati wa taarifa za hali ya hewa hususani taarifa za hali mbaya ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Viktoria’, alibainisha Dkt. Chang’a.

Aliongezea ‘wadau wa mradi huu wakiwemo wataalam kutoka TMA watakaa pamoja na kufanyia maboresho taarifa zinazoatolewa na Mamlaka na hivyo kufanikisha utoaji wa huduma bora zaidi na kusaidia serikali katika jitihada za kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinachangia katika kufanikisha mikakati na jitihada za nchi kufikia uchumi wa kati na uchumi wa viwanda , ‘ 
Awali wakati wa ufunguzi, Bi. Rita Roberts mtaalam wa mradi kutoka ‘National Centre for Atmosphere Research (NCRA)’ alifafanua kuwa mradi huu utasaidia Kanda ya Afrika Mashariki kupitia taasisi zake za hali ya hewa kufanikisha utoaji endelevu wa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa wakati pamoja na kuongeza kiwango cha usahihi na uhakika kwa taarifa za hali ya hewa na hivyo kupunguza athari za vifo na upotevu wa mali.
Mradi huu unahusisha Taasisi za Hali ya Hewa za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na ‘National Centre for Atmosphere Research (NCRA)’ kutoka Marekani, Taasis ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UKMet Office) kwa ufadhili wa ‘Department for International Development (DFID)’ ya Uingereza.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...