Sunday, February 13, 2022
Friday, February 11, 2022
TMA KUENDELEA KUTOA HUDUMA MAHSUSI ZA HALI YA HEWA KWA FAIDA ZA KIUCHUMI.
Dar es Salaam; Tarehe 11
Februari, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), imesema itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma mahususi za hali ya hewa ili kuongeza tija
na ufanisi katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Hayo yalizungumzwa na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mkurugenzi wa Matumizi na Utafiti Dkt. Ladislaus
Chang’a wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Masika
2022 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi katika Ukumbi wa
Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Tarehe 11/02/2022.
“Matumizi sahihi ya taarifa za
hali ya hewa na hasa katika kipindi ambapo dunia inakabiliwa na changamoto ya
mabadiliko ya hali ya hewa na Tabianchi ni muhimu sana na yatasaidia kufikiwa kwa malengo ya mpango wa Taifa wa kujenga uchumi wa viwanda
nchini na mikakati mingine ya kuleta maendeleo katika jamii na Taifa. TMA
itaendelea kuimairisha utoaji wa huduma
mahsusi za hali ya hali ya hewa ili kuhakikisha malengo yanafikiwa”. Alisema
Dkt. Chang’a.
Aidha, katika mkutano huo TMA
ilitoa tathimini ya usahihi wa utabiri wa Msimu wa mvua za vuli 2021 zilizoisha
mwezi Desemba 2021, ambapo tathmini hiyo ilionesha kuwa utabiri ulikuwa sahihi
kwa asilimia 93.8, hivyo mamlaka inaendelea kuweka msisitizo wa matumizi sahihi
ya taarifa za hali ya hewa kwa kila sekta ili kuongeza tija na uzalishaji.
Kwa upande wa mdau kutoka
Wizara ya Kilimo, Bw. Juma Makandi alisema mara baada ya kupata taarifa za
utabiri wa msimu wa mvua za Vuli, Wizara iliaandaa na kutoa tafsiri ya utabiri huo katika shughuli za
kilimo kwa mawaziri pamoja na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kuwawezesha kuweka
mipango stahiki ya kukabiliana na athari za utabiri huo..
Naye, mdau wa Kilimo kutoka
Zanzibar Bw. Nasoro Mkarafuu alieleza kuwa utabiri ulikuwa kama ulivyotabiriwa
hivyo mipango iliyowekwa ya kushirikisha maafisa ugani ilienda kama
ilivyopangwa.
Mdau kutoka ofisi ya Waziri
Mkuu, Idara ya Maafa alisema baada ya kupokea utabiri huo, idara iliandaa kikao
kazi cha kujadili mpango wa dharura wa ukame unaoweza kujitokeza kutokana na
utabiri uliotolewa sambamba na kuandaa vipindi vya elimu kwa umma kupitia
vyombo mbalimbali va habari.
Katika Mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2022 na kuweza kutoa ushauri utaowezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari za utabiri huo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za MASIKA 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 17 Februari 2022.
Tuesday, February 8, 2022
TMA YATAKIWA KUBUNI VYANZO ENDELEVU VYA MAPATO
Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na
Uchukuzi, Dkt. Ally Possy akizungumza wakati
wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, katika ukumbi wa mikutano ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Ally Possy akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi mkuu na wafanyakazi wengine wa TMA baada ya ziara yake Makao Makuu ya Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
Dar es Salaam; Tarehe 07 Februari, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), yatakiwa kubuni vyanzo endelevu vya mapato ili taasisi iweze kujiendesha na kuisaidia serikali katika uendeshaji wake. Hayo yalizungumzwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Ally Possy wakati alipotembelea Ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
“Tusiendeshe Mamlaka kwa hasara, mnatakiwa kubuni vyanzo vya mapato ambavyo vipo “sustainable” bila kuathiri au kuidumaza taasisi, japo tusigeuke kuwa Mamlaka ya ukusanyaji mapato TRA, tutoe huduma lakini pia tukusanye mapato ili kuisaidia serikali katika uendeshaji wake”. Alisema Dkt. Possy.
Katika hatua nyingine, Dkt. Possy aliipongeza TMA kuwa ni taasisi ya tofauti inayofanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na kupelekea kufanya kazi nzuri ya kusaidia maendeleo ya kimkakati na kijamii nchini. Aidha, aliahidi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa TMA pale itakapohitajika.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru wizara na kumueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa Mamlaka imeshaanza kutekeleza jukumu jipya la uratibu na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini.
“ Baada ya kusainiwa kwa kanuni 7 za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, miongoni mwa jitihada kubwa zilizofanywa na Mamlaka ni pamoja na kuanza utekelezaji wa kanuni hizo kwa ajili ya uratibu na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini ikiwa ni jukumu jipya ambalo Mamlaka imekasimiwa”. Alisema Dkt. Kijazi.
Friday, February 4, 2022
UWEPO WA KIMBUNGA “BATSIRAI” KATIKA BAHARI YA HINDI
Dar es Salaam, 04 Februari 2022:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga Batsirai katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi. Mamlaka imeendelea kufuatilia kimbunga hicho tangu kilipojitokeza katika bahari ya Hindi tarehe 27/01/2022 na kwa sasa kimesogea katika maeneo ya kisiwa cha Madagascar.
Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kutokuwepo kwa uwezekano wa kimbunga Batsirai kufika katika Pwani ya Tanzania. Hata hivyo uwepo wa kimbunga Batsirai baharini unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha ongezeko la mvua; vipindi vya upepo mkali unaofika na kuzidi km 40 kwa saa na mawimbi makubwa baharini yanayozidi mita 2 hasa kwa maeneo ya ukanda wa pwani.
Maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa kutokana na uwepo wa kimbunga hicho baharini kati ya tarehe 04 hadi 08/02/2022 ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa. Hata hivyo mvua za Msimu zinaendelea katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na kutoa mrejeo kila itakapobidi.
Friday, January 28, 2022
UTABIRI WA TMA NI WA UHAKIKA.
| Matukio kwa picha wakati Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) akipata ufafanunuzi kutoka vitengo mbalimbali vya TMA wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 28/01/2022. |
| Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) akiwa katika chumba maalum cha kurekodi video za utabiri wa hali ya hewa wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 28/01/2022. |
| Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) akisaini katika daftari la wageni wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 28/01/2022. |
Dar es Salaam; Tarehe 28 Januari, 2022;
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) ametoa rai kwa watanzania kutumia vizuri taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuwa taarifa hizo ni za uhakika. Mhe. Mwakibete, alizungumza hayo wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 28/01/2022.
“kwa niaba ya Serikali na watanzania wengine na mimi binafsi, na kwa niaba ya waziri wangu mwenye kubeba dhamana ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Prof. Mbarawa, niwapongeze sana kwani taarifa zenu zimekuwa za uhakika na ni za kweli”. Alisema. Mhe. Mwakibete.
“Ni rai yangu kwa taasisi zingine na wizara zingine tutumie kikamilifu taarifa zinazotoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, kwa namna hiyo tutakuwa tunaokoa hasara zilizo mbele yetu na kujipanga”. Aliongezea Mhe. Mwakibete.
Akizungumzia suala la changamoto ya maslahi duni, mhe. Waziri alisema kuwa atalisimamia suala hilo kwa kumshirikisha waziri mwenye dhamana na Mamlaka zingine ili kuona namna gani litashughulikiwa ili kuhakikisha wataalamu bingwa wa TMA hawahamia taasisi nyingine.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwakibete alisema, Serikali inatambua umuhimu wa TMA nchini, hivyo Mhe. Rais. Samia Suluhu Hassan kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, ametenga jumla ya Tsh. Bil. 30 ili kukamilisha mtandao wa rada saba nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni taasisi ya Muungano iliyoanzishwa kwa sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ikifanya kazi zake Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar chini ya usimamizi wa Bodi ya TMA (Governing Board).
“Bodi ina jumla ya wajumbe 8, Mwenyekiti na Makamu ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mwenyekiti anatokea Tanzania Bara na Makamu wake anatokea Tanzania Zanzibar, Wajumbe wengine watano (5) wa Bodi ni wateule wa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya hali ya hewa ambapo Katibu wa Bodi hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka. Hawa wajumbe wanawakilisha sekta muhimu zinazotumia taarifa za hali ya hewa”. Alisema Dkt. Nyenzi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alifafanua kuwa Mamlaka imejiwekea malengo yanayolenga kutoa huduma bora zaidi na mahsusi kwa wadau na jamii ili kuchangia katika kutoa maamuzi na hatimaye kuleta maendeleo endelevu.
“Katika kutimiza azma ya Mhe. Rais ya kuwatumikia Watanzania na kutekeleza mipango ya Nchi yetu na ile ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya utoaji wa huduma bora za hali ya hewa nchini, Mamlaka imejipanga kuboresha huduma za hali ya hewa na kuendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini. Aidha mafunzo kwa wafanyakazi na uboreshaji wa mifumo ya menejimenti ya rasilimali fedha itaboreshwa zaidi. Katika kuongeza ubora wa huduma za hali ya hewa, Mamlaka imejiwekea malengo ya kushiriki na kuchangia katika shughuli za hali ya hewa za kitaifa, kikanda na kimataifa hususani katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)”. Alieleza Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi aliishukuru serikali kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kuwa na vitendea kazi vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi ikiwa ni pamoja na kuipatia TMA Rada nyingine mbili ambazo ukamilikaji wake utapelekea kufikiwa kwa malengo ya muda mrefu ya kuwa na Rada 7 za hali ya hewa kwa nchi nzima.
Featured Post
DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.
Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...
-
Dar es Salaam, Tarehe 05/02/2026; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 202 6 kwa maeneo...
-
DODOMA; Tarehe 19 Agosti, 2024; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na...
-
Dar es Salaam, 22 /0 8 /202 4 ; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 202 4 kwa maeneo yanayopat...