Friday, February 4, 2022

UWEPO WA KIMBUNGA “BATSIRAI” KATIKA BAHARI YA HINDI

 



Dar es Salaam, 04 Februari 2022:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga Batsirai katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi. Mamlaka imeendelea kufuatilia kimbunga hicho tangu kilipojitokeza katika bahari ya Hindi tarehe 27/01/2022 na kwa sasa kimesogea katika maeneo ya kisiwa cha Madagascar.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kutokuwepo kwa uwezekano wa kimbunga Batsirai kufika katika Pwani ya Tanzania. Hata hivyo uwepo wa kimbunga Batsirai baharini unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha ongezeko la mvua; vipindi vya upepo mkali unaofika na kuzidi km 40 kwa saa na mawimbi makubwa baharini yanayozidi mita 2 hasa kwa maeneo ya ukanda wa pwani.

Maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa kutokana na uwepo wa kimbunga hicho baharini kati ya tarehe 04 hadi 08/02/2022  ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa. Hata hivyo mvua za Msimu zinaendelea katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na kutoa mrejeo kila itakapobidi.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...