Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na
Uchukuzi, Dkt. Ally Possy akizungumza wakati
wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, katika ukumbi wa mikutano ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Ally Possy akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi mkuu na wafanyakazi wengine wa TMA baada ya ziara yake Makao Makuu ya Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
Dar es Salaam; Tarehe 07 Februari, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), yatakiwa kubuni vyanzo endelevu vya mapato ili taasisi iweze kujiendesha na kuisaidia serikali katika uendeshaji wake. Hayo yalizungumzwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Ally Possy wakati alipotembelea Ofisi za TMA, Makao Makuu, Ubungo Plaza, Tarehe 07/02/2022.
“Tusiendeshe Mamlaka kwa hasara, mnatakiwa kubuni vyanzo vya mapato ambavyo vipo “sustainable” bila kuathiri au kuidumaza taasisi, japo tusigeuke kuwa Mamlaka ya ukusanyaji mapato TRA, tutoe huduma lakini pia tukusanye mapato ili kuisaidia serikali katika uendeshaji wake”. Alisema Dkt. Possy.
Katika hatua nyingine, Dkt. Possy aliipongeza TMA kuwa ni taasisi ya tofauti inayofanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na kupelekea kufanya kazi nzuri ya kusaidia maendeleo ya kimkakati na kijamii nchini. Aidha, aliahidi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa TMA pale itakapohitajika.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru wizara na kumueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa Mamlaka imeshaanza kutekeleza jukumu jipya la uratibu na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini.
“ Baada ya kusainiwa kwa kanuni 7 za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, miongoni mwa jitihada kubwa zilizofanywa na Mamlaka ni pamoja na kuanza utekelezaji wa kanuni hizo kwa ajili ya uratibu na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini ikiwa ni jukumu jipya ambalo Mamlaka imekasimiwa”. Alisema Dkt. Kijazi.
No comments:
Post a Comment