Monday, July 11, 2022

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA HALI YA HEWA NCHINI.




Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika Miundombinu ya Hali ya Hewa Nchini ili kuongeza usahihi wa utoaji wa taarifa ya hali ya hewa kwa wadau wote wakiwemo usafiri wa anga, ulinzi, uvuvi na usafiri wa nchi kavu. 

 

Akizungumza mara baada ya kutembelea rada ya hewa iliyojengwa mkoani Mtwara Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema uhakika wa utabiri  utachangia umakini katika uendelezaji wa miundombinu nchini katika Nyanja zote.

 

“Nawapongeza sana kwa kukamilisha mradi huu na nichukue fursa hii kuwambia wananchi kuwa Serikali tayari iko kwenye hatua mbalimbali za kuongeza rada kufikia saba ili kuhakikisha usahihi wa utabiri unaongezeka’ Amesema Naibu Waziri Mwakibete.

 

Naibu Waziri Mwakibete amesema kuwa pamoja na uwezekezaji huo amewataka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuhakikisha inabuni njia mbalimbali za kutoa taarifa ili kuwafikia wadau wote kwa wakati na kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

 

Naye Mbunge wa Mtwara Mjini. Hassan Mtenga ameiomba Wizara kuijenga barabara inayoingia kwenye miudombinu kuijenga kwa kiwango cha lami kwani barabara hiyo inapata changamoto hasa nyakati za mvua.

 

“Mhe Naibu Waziri Wizara hii ina fedha hebu tizame kwenye bajeti angalau kilomita hizi chache mziwekee lami ili kulinda miundombinu hii mliyoijenga kwa fedha nyingi’ amesisitiza Mbunge Mtenga.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miundombinu wa TMA, Dkt Paschal Waniha… ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miunndombinu ya hali ya hewa na kusema kuwa uwepo wa rada hizo ueanza kuleta mabadiliko hasa kwa wadau wa mikoa ya kusini.

 

Kuhusu utabiri kuwafikia wadau Dkt. Waniha Amesema TMA inatumia njia za ujumbe mfupi na  vyombo vya Habari kuwafikishia taarifa za utabiri wadau wake na imejipanga kuboresha zaidi njia hizo ili kuhakikisha wadau muhimu wanafikiwa.

 

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu kukagua miundombinu mkoani humo.

 

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasilian Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

Monday, July 4, 2022

TAARIFA YA UTENDAJI WA JOPO LA WMO LINALOSIMAMIWA NA DKT. KIJAZI YAWASILISHWA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi (wa pili kutoka kulia kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wengine wa Baraza Kuu la Utendaji wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) wakati wa mkutano wa sabini na tano wa Baraza Kuu la WMO (WMO Executive Council-Seventy Fifth Session) uliofanyika tarehe 20 hadi 24 Juni, 2022, Geneva, Uswisi

Geneva, Uswisi; Tarehe 24/06/2022 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi, Mwenyekiti wa Jopo la WMO la kujenga uwezo wa Nchi Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) “WMO Capacity Development Panel (CDP)”, ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ameshiriki na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya jopo hilo wakati wa Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la WMO “Seventy-Fifth Session of the WMO Executive Council (EC-75)” uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 20 hadi 24 Juni, 2022. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya mikutano iliyotangulia ya WMO ambayo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa 18 wa WMO “Seventeenth WMO Congress (Cg-18)” uliofanyika 2019, Mkutano Mkuu Maalum wa WMO wa 2021 (WMO Extraordinary Congress-2021) na mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la WMO “Seventy-Fourth Session of the WMO Executive Council (EC-74)” uliofanyika 2021. Aidha, Mkutano huo wa 75 wa Baraza la WMO umetoa mapendekezo ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya hali ya hewa na maji yanayotakiwa kutolewa maamuzi na Mkutano Mkuu wa 19 wa WMO “Nineteenth WMO Congress (Cg-19) utakaofanyika mwezi Mei, 2023. 

Akiwasilisha ripoti ya jopo la WMO la kujenga uwezo “WMO Capacity Development Panel (CDP)”, Dkt. Kijazi aliainisha mafanikio yaliyofikiwa kupitia kazi za Jopo hilo ambazo ni pamoja na hatua zilizofikiwa za mapitio ya miongozo ya mafunzo ya wataalamu wa hali ya hewa “Status of the review of Basic Instructional Packages(BIPs)”; Uundwaji wa chombo kitakachowaunganisha wadau wote wanaotoa elimu ya hali ya hewa na maji “Consortium of WMO Education and Training Partners (CONECT)”; Mapitio ya mpango mkakati wa mafunzo wa WMO “Review the WMO Capacity Development Strategy (CDS)”; Maandalizi ya mwongozo wa kuhakikisha kuwa kazi za utoaji wa taarifa za hali ya hewa zinaendelea hata kipindi ambacho majanga kama UVIKO-19 yanapojitokeza, “Business Continuity and Contingency Planning Guidance”; Chapisho jipya la WMO la kisera na uongozi hasa likilenga taasisi za hali ya hewa “New publication on Public Policy and Management with focus on NMHSs”; Pamoja na ushirikiano kati ya sekta za hali ya hewa na maji kupitia Jopo la uratibu wa sekta za WMO, “Collaborations with the Hydrological Coordination Panel” 

 Aidha, Dkt. Kijazi alishiriki katika mkutano wa wa tatu wa Jukwaa la WMO la Kutoa Maoni “Third High-Level Session of Open Consultative Platform (OCP-HL-3)”), uliofanyika tarehe 20 Juni 2022 ambapo alikuwa Mwanajopo “Panelist”. Wakati akitoa mada na kujibu hoja kuhusiana na vipengele muhimu vya kisera na kisheria vya kuzingatiwa ili kukidhi mahitaji na majukumu ya taasisi za hali ya hewa kuendana na wakati, Dkt.Kijazi alisema “TMA ipo kisheria na kazi zake zimeainishwa katika Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, kifungu namba 5, ambapo TMA imepewa dhamana ya kutoa huduma za hali ya hewa ikijumuisha za kibiashara na zisizo za kibiashara pamoja na kudhibiti (regulate) huduma hizo katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” 

Aidha, akiendelea kufafanua juu ya matakwa ya sheria hiyo alisema kuwa, sheria inawataka wadau wanaotumia huduma za hali ya hewa kwa shughuli za biashara kuchangia gharama kidogo ili ziwe endelevu kwa kuboresha miundo mbinu ambayo kwa hivi sasa kwa kiasi kikubwa inagharamiwa na serikali. Kwa kuongezea, Dkt.Kijazi alitoa wito kwa WMO kuongeza juhudi na rasilimali katika kuzisaidia taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wenye uwezo mdogo hususan katika Bara la Afrika na Asia ili ziweze kutoa huduma za hali ya hewa kwa viwango vinavyokubaliwa na WMO. Mkutano wa WMO EC-75 ulitanguliwa na Mkutano wa 41 wa Kamati ya Ushauri ya WMO katika Masuala ya Fedha “WMO Financial Advisory Committee (FINAC- 41) ambao pia Dkt. Kijazi ni mjumbe uliofanyika tarehe 16 na 17 Juni 2022, Geneva- Uswisi. 

Baraza Kuu la WMO ni chombo chenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa WMO (WMO Congress). Baraza hili linaundwa na wajumbe 37 wawakilishi kutoka mabara yote ya Dunia kwa uwiano uliopitishwa na Mkutano Mkuu wa WMO. Hivyo Baraza Kuu la WMO linaundwa na Rais wa WMO, Makamu wa Kwanza wa Rais; Makamu wa Pili wa Rais, Makamu wa Tatu wa Rais, Marais wa kanda sita(6) za WMO (WMO Regional Associations), na wajumbe 27 ambao ni Wakuu wa taasisi mbalimbali za hali ya hewa. Wawakilishi kutoka Kanda ya Afrika “WMO Regional Association 1(RA 1) kwa sasa ni: Makamu wa Tatu wa Rais, Dkt. Agnes Kijazi (Tanzania), Rais wa RA I, Dkt. Daouda Konate (Cote d'Ivoire) na wajumbe saba (7) kutoka nchi za Msumbiji, Chad, Morocco, Nigeria, Cameroon, Ethiopia na Namibia.

Friday, June 3, 2022

TAARIFA POTOFU INAYOSAMBAA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU HALI YA BARIDI HAPA NCHINI


 

Dar es Salaam, Tarehe 03 Juni 2022:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa potofu kuhusu hali ya baridi inayoendelea nchini. Taarifa hiyo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza, “kuanzia kesho hadi Agosti 22 mwaka huu kutakuwa na baridi zaidi kuliko miaka ya nyuma”. Taarifa hiyo potofu imehusisha Aphelion. Tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa dunia kwenye mfumo wa jua (solar system). Hata hivyo, mchango wake katika mwenendo wa hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine ni mdogo katika maeneo yetu kutokana na kuwa karibu na Ikweta.

Kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti kila mwaka, ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi hapa nchini ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali. Utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa na TMA tarehe 1 Juni 2022 unaonesha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Viwango vya joto la chini vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 140C hadi 260C kwa maeneo ya ukanda wa pwani, kati ya nyuzi joto 40C hadi 140C kwa maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi na kati ya nyuzi joto kati ya 100C hadi 200C kwa maeneo mengine ya nchi. Aidha, TMA imetoa tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa. Tahadhari hiyo ni kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Alhamisi tarehe 2 na inatarajiwa kudumu hadi tarehe 6 Juni 2022 na ambayo itakuwa ikihuishwa kila inapobidi.

TMA inapenda kuwakumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, TMA ndio taasisi pekee yenye jukumu la kutoa taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa Umma na kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa kutoka katika vyanzo visivyo rasmi kwa mujibu wa kifungu cha 27 na 31(5) cha Sheria hiyo.

Wednesday, June 1, 2022

KIPUPWE 2022: SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUCHUKUA TAHADHARI YA VIPINDI VYA BARIDI NA UPEPO MKALI VINAVYOWEZA KUJITOKEZA.


 

Dar es Salaam, Tarehe 01/06/2022

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2022. Taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, alisisitiza sekta mbalimbali kuchukua tahadhari za vipindi vya baridi na upepo mkali vinavyoweza kujitokeza nchini.

“Katika kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi ya nchi, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa mwezi Juni na Julai huku vipindi vya baridi kali vikitarajiwa katika maeneo yenye miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi, hivyo ni vyema sekta mbalimbali kuchukua tahadhari ya athari zinazoweza kujitokeza”. Alisisitiza Dkt. Chang’a

Dkt. Chang’a aliongezea kuwa hali ya joto la bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la bahari, kusini-mashariki mwa bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) hali inayotarajiwa kusababisha ukavu katika msimu huo, japo upepo unaotarajiwa kuvuma kutoka kusini mashariki na mashariki unaweza kuleta unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani).

Aidha, jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kuzingatia tahadhari za upepo mkali zitakazotolewa na TMA pale zitakapojitokeza.

Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...