Monday, July 11, 2022

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA HALI YA HEWA NCHINI.




Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika Miundombinu ya Hali ya Hewa Nchini ili kuongeza usahihi wa utoaji wa taarifa ya hali ya hewa kwa wadau wote wakiwemo usafiri wa anga, ulinzi, uvuvi na usafiri wa nchi kavu. 

 

Akizungumza mara baada ya kutembelea rada ya hewa iliyojengwa mkoani Mtwara Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema uhakika wa utabiri  utachangia umakini katika uendelezaji wa miundombinu nchini katika Nyanja zote.

 

“Nawapongeza sana kwa kukamilisha mradi huu na nichukue fursa hii kuwambia wananchi kuwa Serikali tayari iko kwenye hatua mbalimbali za kuongeza rada kufikia saba ili kuhakikisha usahihi wa utabiri unaongezeka’ Amesema Naibu Waziri Mwakibete.

 

Naibu Waziri Mwakibete amesema kuwa pamoja na uwezekezaji huo amewataka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuhakikisha inabuni njia mbalimbali za kutoa taarifa ili kuwafikia wadau wote kwa wakati na kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

 

Naye Mbunge wa Mtwara Mjini. Hassan Mtenga ameiomba Wizara kuijenga barabara inayoingia kwenye miudombinu kuijenga kwa kiwango cha lami kwani barabara hiyo inapata changamoto hasa nyakati za mvua.

 

“Mhe Naibu Waziri Wizara hii ina fedha hebu tizame kwenye bajeti angalau kilomita hizi chache mziwekee lami ili kulinda miundombinu hii mliyoijenga kwa fedha nyingi’ amesisitiza Mbunge Mtenga.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miundombinu wa TMA, Dkt Paschal Waniha… ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miunndombinu ya hali ya hewa na kusema kuwa uwepo wa rada hizo ueanza kuleta mabadiliko hasa kwa wadau wa mikoa ya kusini.

 

Kuhusu utabiri kuwafikia wadau Dkt. Waniha Amesema TMA inatumia njia za ujumbe mfupi na  vyombo vya Habari kuwafikishia taarifa za utabiri wadau wake na imejipanga kuboresha zaidi njia hizo ili kuhakikisha wadau muhimu wanafikiwa.

 

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu kukagua miundombinu mkoani humo.

 

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasilian Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...