Wednesday, September 16, 2026

DKT CHANG’A NA KATIBU MKUU WMO WAZUNGUMZIA HALI YA EL NINO YA 2026

 


Geneva: 15 Septemba, 2026

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a alikutana na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Prof. Celeste Saulo na kufanya mazungumzo kuhusu uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, hali ya El Nino 2026 na umuhimu wa kuendelea kuimarisha utoaji wa taarifa za mapema na maandalizi ya kukabiliana na athari zake. 



Prof. Saulo alimpongeza Dkt. Chang’a na kufurahishwa na namna TMA wanavyoendelea kusimamia vyema utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania hususan katika kutoa elimu na kutahadharisha Umma na Wadau mbalimbali kuhusiana na hali ya El Nino na athari zake katika misimu ya mvua.  Aidha, Prof. Saulo ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za hali ya hewa kupitia programu mbalimbali za WMO ikiwa ni pamoja na eneo la matumizi ya akiliunde (AI) katika mnyororo mzima wa utoaji wa huduma za hali ya hewa. 


“Napongeza juhudi za Tanzania katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na elimu hususan katika kipindi hiki tunachokabiliwa na Hali ya El Nino yenye nguvu. Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa na nimetumia Tanzania kama mfano mzuri wa utoaji wa elimu kuhusu El Nino na maandalizi ya kukabiliana na hali hiyo katika hotuba yangu ya hivi karibuni kuhusiana na hali inavyoendelea” Alisema Prof. Celeste Saulo.


Katika Kikao hicho, Dkt.Chang’a alimshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa kuendelea kuiamini Tanzania na TMA na kuendelea kuisaidia TMA kupitia programu zake mbalimbali za uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kikanda na kitaifa ambazo zinatekelezwa kwa ushirikiano na Wadau wa Maendeleo na Nchi Wanachama wa WMO ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri. 


“Naendelea kushukuru sana kwa usaidizi wa WMO kupitia programu zake mbalimbali ambazo zinachangia pakubwa katika kuboresha huduma na utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini na nchi nyingine pia kuongeza nguvu katika uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya hali ya hewa”.


Aidha, Dkt. Chang’a alimjulisha Katibu Mkuu wa WMO kuwa, kupitia programu za WMO, Tanzania imeweza kusaidia wataalamu wa hali ya hewa wa nchi nyingine kwa kutoa msaada wa kiufundi na miongoni mwa nchi hizo ni  Seychelles, Burundi, Sudan Kusini, na Namibia. Maeneo ambayo TMA imezisaidia nchi nyingine katika tasnia hii ya hali ya hewa ni pamoja na maeneo ya uboreshaji wa “Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa huduma na Umahiri wa Wataalamu (Quality Management System-QMS and Competency Assessment )”, “Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa (Severe Weather Forecasting)”, “Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Kutumia Modeli za Kompyuta (Numerical Weather Prediction-NWP)”, “Mchakato wa kisheria katika sekta ya hali ya hewa (Legal Matters)” na Usambazaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Umma (Public Weather Services-PWS). 

Vilevile Dkt. Chang’a alimshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa fursa ya kuleta mikutano mikubwa ya kitaalamu nchini ikiwa ni pamoja na mkutano wa nne (4) wa wataalamu wa matumizi ya huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi “The Fourth WMO Operational Climate Prediction (OCP-4)” uliofanyika Arusha mwishoni mwa mwezi Juni hadi mwanzo wa Julai 2026 kwa mara ya kwanza barani Afrika na kwa Tanzania na kwa ufanisi mkubwa. Tanzania , kupitia TMA itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa nne wa wataalamu wabobezi wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi IPCC (IPCC WG1-LAM3) unaotarajiwa kufanyika Arusha mwanzoni mwa mwezi Novemba 2026.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...