Dar es Salaam, Tarehe 03 Juni 2022:
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa potofu
kuhusu hali ya baridi inayoendelea nchini. Taarifa hiyo imesambaa kwenye
mitandao ya kijamii ikieleza, “kuanzia kesho hadi Agosti 22 mwaka huu kutakuwa
na baridi zaidi kuliko miaka ya nyuma”. Taarifa hiyo potofu imehusisha Aphelion.
Tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa dunia kwenye
mfumo wa jua (solar system). Hata hivyo, mchango wake katika mwenendo wa
hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine ni mdogo katika maeneo yetu
kutokana na kuwa karibu na Ikweta.
Kipindi
cha miezi ya Juni hadi Agosti kila mwaka, ni majira ya Kipupwe katika maeneo
mengi hapa nchini ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi na
upepo mkali. Utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa na TMA tarehe 1 Juni 2022 unaonesha
kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi
ya nchi. Viwango vya joto la chini vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 140C
hadi 260C kwa maeneo ya ukanda wa pwani, kati ya nyuzi joto 40C
hadi 140C kwa maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi na kati ya
nyuzi joto kati ya 100C hadi 200C kwa maeneo mengine ya
nchi. Aidha, TMA imetoa tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na
mawimbi makubwa. Tahadhari hiyo ni kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya
Bahari ya Hindi kuanzia Alhamisi tarehe 2 na inatarajiwa kudumu hadi tarehe 6 Juni
2022 na ambayo itakuwa ikihuishwa kila inapobidi.
TMA
inapenda kuwakumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa,
Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, TMA ndio taasisi pekee yenye jukumu la kutoa
taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa Umma na kuwa ni kosa
kisheria kusambaza taarifa kutoka katika vyanzo visivyo rasmi kwa mujibu wa
kifungu cha 27 na 31(5) cha Sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment