Dar es Salaam, Tarehe
01/06/2022
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa
Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2022. Taarifa hiyo imeelezea
athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali
wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza
na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, alisisitiza
sekta mbalimbali kuchukua tahadhari za vipindi vya baridi na upepo mkali
vinavyoweza kujitokeza nchini.
“Katika
kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali
vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi ya nchi, vipindi vya baridi zaidi
vinatarajiwa mwezi Juni na Julai huku vipindi vya baridi kali vikitarajiwa
katika maeneo yenye miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati
za usiku na asubuhi, hivyo ni vyema sekta mbalimbali kuchukua tahadhari ya
athari zinazoweza kujitokeza”. Alisisitiza Dkt. Chang’a
Dkt. Chang’a aliongezea kuwa hali ya joto la
bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la
bahari, kusini-mashariki mwa bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) hali
inayotarajiwa kusababisha ukavu katika msimu huo, japo upepo unaotarajiwa kuvuma kutoka kusini mashariki na mashariki
unaweza kuleta unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vya
mvua nyepesi katika maeneo machache ya Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na
pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani).
Aidha,
jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari
zinazoweza kujitokeza pamoja na kuzingatia tahadhari za upepo mkali
zitakazotolewa na TMA pale zitakapojitokeza.
Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast
No comments:
Post a Comment