Tuesday, August 30, 2022

WILAYA 86 NCHINI KUNUFAIKA NA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2022.











Dar es Salaam; Tarehe 30 Agosti, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema imeendelea kuongeza wigo wa utoaji taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo, ambapo msimu wa Vuli 2022 utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita zilizo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa ziwa Viktoria. Hayo yalizungumzwa na Mwenyekeiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Tarehe 30/08/2022.

 

Utabiri huu wa msimu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Viktoria. Hivyo, mimi binafsi napenda kutoa pongezi nyingi sana kwa hatua hii kubwa ya kuongeza wigo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa hususan kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wa sekta na maeneo mbalimbali ambao wamekuwa na uhitaji wa taarifa hizi kwenye maeneo yao”. Alisema Dkt. Nyenzi.

 

Aidha, Dkt Nyenzi alisisitiza ushirikiano katika kuhakikisha kwamba taarifa hizo zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuleta tija pamoja na kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta zao.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Matumizi Sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa Maendeleo Endelevu” hivyo, katika kuendana na kaulimbiu hiyo, TMA imeendelea kuboresha taarifa zake kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali na kuongeza thamani katika taarifa zake za utabiri wa msimu kwa kujumuisha taarifa za maeneo madogo madogo kwa ngazi ya wilaya.

“Wakati Serikali ya awamu ya sita ikiendelea na jitihada za kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kuweka msisitizo wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa kila sekta ili kuongeza tija katika uzalishaji”.Alizungumza Dkt. Kijazi.

Kwa upande wa mdau kutoka Wizara ya Kilimo, akizungumzia utabiri wa msimu uliopitaBw. Juma Makandi alisema mara baada ya kupata taarifa za utabiri wa msimu wa mvua za Masika za awali na zilizohuishwa, wizara iliaandaa tafsiri ya utabiri huo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwasilisha kwa wadau mbalimbali kwa utekelezaji wake.

Katika Mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 na kuweza kutoa ushauri utaowezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari (hasi au chanya) za utabiri huo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 1 Septemba 2022.


 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...