Mbeya; Tarehe 05 Agosti,
2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), imehimizwa kuongeza jitihada za kuifikishia jamii taarifa za hali ya hewa kwa wakati, hayo yalizungumzwa
na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema akimuwakilisha Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas alipotembelea banda la TMA,
tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika
katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8
Agosti, 2022.
“Kazi yenu inajitangaza kwa
kuwa mmekuwa mnafanya vizuri katika utabiri wenu wa msimu hivyo nawapongeza
sana, lakini niwahimize kuongeza jitihada za kuwafikishia jamii taarifa hizo za
hali ya hewa kwa wakati ziweze kutumika na kuwasaidia kwa wakati. Alisisitiza
Mhe. Pololet Mgema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo akiongozana na Mhe. Pololet Mgema aliongezea kwa
kuipongeza TMA kwa utabiri mzuri wanaoutoa na kufanya wananchi kuwa na imani na
taarifa za hali ya hewa kwa kuzitumia katika shughuli zao za kiuchumi na
kijamii.
Aidha, akielezea namna TMA
ilivyoboresha utabiri wa hali ya hewa katika ngazi ya wilaya kupitia vyombo vya
habari, Ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo alisema,
Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Namba 2 ya mwaka 2019 imeipa
Mamlaka jukumu la kutoa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na tayari imeshaboresha vifaa na
mitambo ya hali ya hewa inayotumia teknolojia ya kisasa inayosaidia upatikanaji
wa taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi zinazokusanywa katika vituo vya hali
ya hewa ikiwemo kituo cha hali ya hewa kinachojiendesha chenyewe (Automatic
Weather Station-AWS) ambacho kimeletwa kwenye maonesho hayo.
Ndg. Isack Yonah aliongezea
kuwa katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, TMA inatoa utabiri wa hali ya
hewa hadi ngazi ya wilaya na hata kama ikitokea mkulima au mdau yeyote
atahitaji kujua hali ya hewa ya eneo lake anaweza kuandaliwa taarifa mahususi
kulingana na mahitaji yake kwa kuchangia huduma hiyo ili kufanya huduma hizo
ziendelee kuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment