Mgeni rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya
Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wanahabari wa Utabiri
wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa TARI, Kibaha, Tarehe 31/08/2022. |
Meneja Mitambo na miundombinu wa TMA Ndugu. Samwel Mbuya akiongea na wanahabari katika Mkutano wa wanahabari wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa TARI, Kibaha, Tarehe 31/08/2022. |
Matukio katika picha wakati waandishi wakisikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa katika Mkutano wa wanahabari wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa TARI, Kibaha, Tarehe 31/08/2022. |
Tarehe 31 Agosti, 2022; Kibaha
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi, amewataka wanahabari kutoa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zilizosahihi haswa kwa maeneo ya ziada ya kisekta kutoka kwa wataalamu ili taarifa iweze kuifikia jamii kwa ukamilifu. Aliyasema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa wanahabari wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa TARI, Kibaha, Tarehe 31/08/2022.
“Napenda kuwakumbusha kufikisha taarifa hizi kwa usahihi na kutafuta, kupata na kuwasilisha ufafanuzi na maeneo ya ziada ya kisekta kutoka kwa wataalamu ili taarifa iweze kuifikia jamii kwa ukamilifu”. Alisema Dkt. Kijazi
Dkt.Kijazi alisema kuwa taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi na za uhakika zitaisaidia jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Pia zitazisaidia Mamlaka zinazohusika kupanga mipango ya kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa, upatikanaji wa chakula na lishe bora pamoja na afya kwa ustawi wa jamii na hivyo kuchangia katika maendeleo endelevu.
Aidha, wakati akiendelea kusema hayo, aliongezea kuwa kupatikana kwa utabiri wa msimu wa Vuli 2022 kwa usahihi na kwa wakati kutachangia katika jitihada za seriakali ya awamu ya sita katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, nchi kwa ujumla pamoja na kuboresha miundombinu na huduma za kijamii hapa nchini.
Kwa upande wake David Gumbo, mwandishi kutoka EATV akizungumza kwa niaba ya waandishi aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa vyombo vya habari ambao umesaidia kutoa taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi na kwa wakati kwa jamii.
Katika Mkutano huo, wahabari walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 na kujadili na kupata uelewa wa pamoja ili kurahisisha uwasilishwaji wa utabiri huu kwa jamii kwa ufanisi na katika lugha inayoeleweka kirahisi pindi utakapotolewa rasmi Tarehe 02 Septemba,2022.
No comments:
Post a Comment