Tuesday, August 2, 2022

TANZANIA YAZINDUA RASMI MRADI WA KUBORESHA TEKNOLOJIA YA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI












Dar es Salaam; Tarehe 02 Agosti, 2022;

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imezindua rasmi mradi wa FINKERAT unafadhiliwa na Serikali ya Finland ambao unalenga kuboresha teknolojia ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini. Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Fredy Mwakibeta (MB) katika Ubalozi wa Finland, Dar es Salaam, tarehe 02/08/2022.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mwakibete alisema, Mradi wa FINKERAT unatarajia kuboresha huduma za hali ya hewa kwa kuhakikisha zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya Taifa.

“Ni matarajio yangu kuwa utekelezaji wa mradi huu utasaidia huduma za hali ya hewa kuwafikia watumiaji katika viwango vya ubora na kwa wakati ili kuwawezesha kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoathiri shughuli za kijamii na kiuchumi”. Alizungumza Mhe. Mwakibete. 

Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Riita Swan alieleza kuwa Finland na Tanzania wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu, hivyo utekelezaji wa mradi huu utaleta mchango mkubwa kwenye kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo misitu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na  Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru serikali ya Finland kwa kufadhili mradi huo. alisema kuwa mradi huo utasaidia kutatua changamoto ya  kwendana na kasi ya kukua kwa teknolojia inayozikabili Taasisi nyingi za Hali ya Hewa dunia hususan nchi zinazoendelea.

 

“Kupitia mradi huu, tunatarajia kununua mtambo wa kisasa wa ‘SmartMet’ na ‘Smartmet Alert’ ambao utawezesha Mamlaka kupata taarifa za hali ya hewa za muda huohuo (real-time) hivyo utachangia katika kurahisisha utoaji tahadhari za hali mbaya ya hewa katika viwango vya juu na teknolojia ya kisasa, aidha, utasaidia pia kuboresha shughuli za uangazi, uhifadhi, uchakataji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kisasa zaidi”. Alisema Dkt. Kijazi

 

Awali wakati akitoa maelezo mafupi ya mradi wa FIKERAT (Finland, Kenya, Rwanda and Tanzania), mwakilishi kutoka Taasis ya Hali ya Hewa Finland (FMI), Bw. Harri Pietarila alisema mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Finland na unategemea kutekelezwa katikati nchi za Kenya, Rwanda na Tanzania kwa kushirikiana na FMI, ukilenga kuboresha huduma za hali ya hewa katika nchi hizo na kufanikisha utekelezaji wa mipango mkakati ya Taasisi za nchi husika.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...