Dar es Salaam; Tarehe 30/06/2022
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi, ambaye pia ni
Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amewataka
wafanyakazi wanaofanya kazi katika ofisi za TMA zilizopo katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA),
kutumia sheria ya Mamlaka katika kukusanya mapato yatakayochangia katika
uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini. Aliyasema hayo alipokuwa akifunga
rasmi mafunzo ya siku nne yanayohusiana na uangazi wa anga la juu pamoja na taratibu
za udhibiti wa ubora “Quality Management Systsem (QMS) procedures”, katika ofisi
za TMA - JNIA, tarehe 30 Juni 2022.
“Nimekuwa nasisitiza muda mrefu juu ya kufanya kazi
kwa ushirikiano yaani “Team work” hali iliyotuwezesha kutufikisha mpaka
tukapata sheria yetu ya Mamlaka, lakini sasa siongelei tena “Team work” kwani
najua hiyo ipo tayari katika utendaji kazi wetu wa kila siku, lakini hivi sasa nazungumzia
suala la mapato, tunatakiwa tuitumie sheria yetu ya Mamlaka vizuri katika ukusanyaji
wa mapato yatakayochangia kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini”.
Alisisitiza Dkt. Kijazi.
Aidha, Dkt. Kijazi aliwapongeza wafanyakazi kwa
kupata mafunzo hayo kwani
yatawaongezea uelewa katika utendaji kazi wao wa kila siku sambamba na kupata nafasi
ya kujikumbusha masuala ya QMS, kwa lengo hilo hilo la kuboresha huduma za hali
ya hewa hususan kwa usalama wa usafiri wa anga.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja wa TMA, Kituo cha Hali ya Hewa JNIA
Bw. John Mayunga alimshukuru Mkurugenzi
Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi pamoja na menejiment yake kwa ujumla kwa
kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu ya siku nne, ambapo yalijumuisha kujifunza
namna ya kutafsiri taarifa zinazotokana na uangazi wa anga za juu pamoja na
namna ya kufanya kazi kwa kufuata taratibu za QMS. Aidha, kwa upande wa
wafanyakazi wa TMA wa JNIA walimpongeza Dkt. Kijazi kwa utendajikazi wake mzuri
kitaifa na kimataifa.
No comments:
Post a Comment