Tuesday, July 12, 2022


Dar es Salaam; Tarehe 01/07/2022

Data za hali ya hewa kwa anga la juu ni muhimu sana katika uandaaji wa utabiri wa hali ya hewa, kwani huonesha hali ya anga kwa mwelekeo wa kwenda juu yaani “Vertical Profile” hali hiyo hutoa viashiria kuhusu hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa yaani ambayo husaidia katika kuhakikisha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unakuwa bora zaidi” Alieleza hayo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi, ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alipokuwa akizindua kituo cha uangazi wa anga la juu kilichopo katika ofisi za TMA zilizopo Uwanja wa Ndege wa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere – Dar es Salaam, tarehe 30 Juni 2022.

Dkt. Kijazi alisema uwepo wa vifaa hivyo utasaidia upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa za anga la juu ambazo ni muhimu sana katika utabiri wa hali ya hewa unaosaidia shughuli za kijamii na kiuchumi hususan usafiri wa anga. Aidha, katika kuhakikisha uangazi wa hali ya hewa kwa anga la juu unaendelea, TMA imeweka malengo ya kufufua na kuanzisha vituo vingine vipya vya kupima anga la juu (Upper Air) kwa kuhusisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa programu za kikanda na kimataifa za mashirikiano katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, ambapo kituo hicho cha kupima anga la juu kilichozinduliwa  kimepatikana kupitia mradi wa hali ya hewa wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) wa kuboresha huduma za hali ya hewa katika eneo la Afrika Mashariki kwa maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria uliopewa jina la High Impact Weather Lake System (HIGHWAY). Mwisho Dkt. Kijazi aliwaagiza watendaji kuhakikisha wanasimamia mitambo hiyo ipasavyo kwa kutatua changamoto pale zinapojitokeza na kuhakikisha taarifa hizo muhimu zinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wa mtaalamu wa ufundi anayesimamia mtambo huo, Bw. Nassoro Nguzo, alitoa taarifa kuwa mtambo huo ni wa kisasa na una uwezo wa kuzalisha gesi ya hydrojeni wenyewe (Automatic) na pindi ikitokea hitilafu sehemu yoyote ya mtambo, ikiwa ni pamoja na kuvuja kwa gesi katika mtambo au mitungi ya kuhifadhia gesi hiyo, basi mtambo una uwezo wa kugundua hitilafu husika, kupiga kengele (alarm), kusimamisha uzalishaji wa gesi na kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa mtaalamu msimamizi wa mtambo. Mfumo huo unasaidia na kurahisisha uendeshaji wa mtambo, ufanisi wa kazi na usalama wa wataalamu.

Katika taarifa yake fupi Meneja wa kituo cha Hali ya Hewa cha Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Bw. John Mayunga alielezea namna ofisi ilivyojipanga katika kuhakikisha wananchi wa maeneo Jirani na kituoni hapo wanapata uelewa kupitia namba za simu walizoziandika katika kifaa hicho cha kupima taarifa za hali ya hewa kwa anga la juu (Sondes) na kuwatoa hofu pale kinapoangukia katika makazi yao.

 

Aidha, Bi. Mecklina Merchades, Mtaalamu wa hali ya hewa wa TMA akitoa maelezo mafupi juu ya utekelezaji wa mradi wa HIGHWAY hapa nchini kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa Dkt. Ladislaus Changa alisema kuwa, moja ya matokeo ya utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na ufufuaji wa mtambo huo wa TMA uliopo JNIA wa kupima taarifa za hali ya hewa za anga la juu .

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...