Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi,
amekabidhiwa ufunguo wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani na Mstahiki Meya
wa Jiji hilo Bw. William E. Cooper alipowatembelea
wataalamu kutoka TMA na mjumbe kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) wanaoshiriki
katika zoezi la kuhakiki utendaji kazi wa radar za hali ya hewa (“Factory
Acceptance Test (FAT)”) katika kiwanda cha Enterprise Electronics
Corporation-EEC kilichopo katika Jiji la Enterprise, kuanzia tarehe 18 hadi 29
Julai, 2022.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mstahiki
Meya Cooper alisema amefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya EEC na TMA
katika eneo la ununuzi na matengenezo ya Rada za Hali ya Hewa, na kuwakaribisha
katika mji wa Enterprise. Kwa heshima ya ushirikiano huo, Mstahiki Meya
alimkabidhi Dkt Kijazi Ufunguo wa Jiji la Enterprise ikiwa ni heshima ya pekee
kuwa anakaribishwa katika Jiji la
Enterprise.
“Nakukabidhi ufunguo huu kama alama ya
heshima unayopewa katika jiji la Enterprise kwamba unaweza kuingia na kutoka
upendavyo, aidha, umjulishe Balozi wa Marekani nchini Tanzania kuhusu wewe
kupatiwa ufunguo huu”. Alisema Bw. Cooper.
Aidha, Mstahiki Meya pia alimpatia zawadi
ya sanamu ya kumbukumbu ya historia ya Jiji la Enterprise yenye kuelezea namna
mdudu mharibifu wa zao la pamba (boll weevil) alivyobadilisha shughuli za
kilimo za eneo la Enterprise kutoka kilimo cha zao la pamba miaka ya 1800 hadi
1900 na kugeukia kilimo cha zao la karanga ambalo limekuwa na manufaa makubwa
katika uchumi wa jiji la Enterprise.
“Mabadiliko hayo yamefanya mdudu huyu
aheshimiwe kwamba kupitia uharibifu wake amesababisha mageuzi yenye mafanikio
katika sekta ya kilimo.Ukipita katika baadhi ya maeneo ya jiji hili la
Enterprise utaona sanamu hii ambayo ina historia muhimu katika mageuzi ya
kilimo katika jiji hili”. Alieleza Bw. Cooper.
Kwa upande wake, Dkt. Kijazi
alimshukuru Mstahiki Meya Cooper kwa kutenga muda wake na kuja kuwasalimia
wakati wa zoezi hilo la ukaguzi wa matengenezo ya mitambo miwili ya Rada za
hali ya Hewa zitakazofungwa mkoani Songwe na Kigoma, Rada ambazo zimegharamiwa
na Serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment