Tuesday, July 26, 2022

MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA HUJENGA UHIMILIVU WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

Dar es Salaam, Tarehe 20/07/2022: 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau wa kilimo katika warsha ya kujenga uelewa wa sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya TMA na kanuni ya uchangiaji na utoaji wa huduma za hali ya hewa mahususi kwa sekta ya kilimo nchini. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, TMA alieleza kuwa matumizi ya taarifa za hali ya hewa yanasaidia kujenga uhimilivu katika sekta zote hasa kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. 

“Tunaona jinsi mabadiliko ya hali ya hewa yanavyotokea, hususan matukio ya hali mbaya ya hewa kama mvua kubwa za muda mfupi ambazo zinaleta athari na kuwepo kwa matukio ya ukame ambayo ni makubwa na yanajirudia kulinganisha na miaka ya nyuma ambayo yanaathiri utekelezaji katika sekta ya kilimo. Ili kuweza kukabiliana na hiyo hali na kujenga uhimilivu katika sekta zote hasa sekta ya kilimo, matumizi ya taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana”.

Kwa upande wake Meneja Huduma za Hali ya Hewa Kilimo kutoka TMA, Bw. Isack Yonah alisema ni muhimu mkulima kupata taarifa za hali ya hewa kabla ya msimu kuanza, wakati msimu unaendelea na mwisho wa msimu ambapo itamsaidia mkulima katika uandaaji wa shamba, kuchagua zao la kulima, wakati wa kupanda na kufanya parizi, kuvuna na kuhifadhi mazao, kutafuta masoko n.k.

Naye Mwanasheria kutoka TMA, Bw. Emmanuel Ntenga alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imepewa majukumu matatu ambayo ni kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii. Hii ni kutokana na kukua kwa sekta ya hali ya hewa, kuongezeka kwa wadau wanaomiliki vituo vya hali ya hewa na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za hali ya hewa nchini. 

Warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 20 Julai, 2022, ikiwajumuisha wadau kutoka sekta ya kilimo, sekta ya uchukuzi na wataalam kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...