Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa juu ya hali ya ongezeko la
joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Kwa kawaida kipindi cha miezi ya
Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha
kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha
kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi
mingine. Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni
mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya
Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa
linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto
kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu
zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
Nyakati za usiku pia kunaonekana kuwa na
hali ya joto kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani
kinachofika asilimia themanini na zaidi kwa baadhi ya maeneo. Unyevunyevu huo
hutunza hali ya joto litokanalo na mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto.
Katika kipindi hiki cha mwezi Disemba, 2020 upungufu wa mvua unatarajiwa
kujitokeza katika baadhi ya maeneo yanayopata mvua za Vuli (ukanda wa ziwa
Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini). Hali
hii inatarajiwa kuendelea kusababisha uwepo wa hali ya joto katika maeneo hayo.
Hata hivyo, hali ya joto inatarajiwa kupungua kidogo katika kipindi cha mwezi
Januari, 2021 kutokana na mvua zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo. Aidha,
vipindi hivi vya joto vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwezi Februari
2021 wakati jua litakapokuwa la utosi hapa nchini.
Baada ya kipindi hicho hali
ya joto inatarajiwa kuanza kupungua hasa kuelekea mwezi Machi ambapo mtawanyiko
wa mvua unatarajiwa kuongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu na kuanza
kwa msimu wa mvua za masika.
Taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa
katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, hivyo tunatoa
wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki
kila inapobidi.
No comments:
Post a Comment