Wadau kutoka wilaya ya Handeni mkoani Tanga wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Toba Nguvila kwenye warsha ya kuongeza uelewa wa upatikanaji, kutafsiri matumizi na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa katika ukumbi wa FDC, Handeni
Handeni, Tanga; Tarehe 19 Disemba, 2020;
DC HANDENI: TAARIFA ZA HALI YA HEWA NI NYENZO MUHIMU KATIKA UCHUMI WA TAIFA.
Handeni, Tanga; Tarehe 19 Disemba, 2020;
Wananchi wa Handeni, mkoani Tanga wametakiwa kutumia taarifa za hali ya hewa katika kuleta mafanikio ya kiuchumi kwa Taifa letu. Hayo yalizungumzwa na Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Toba Nguvila wakati akifungua rasmi Warsha ya Kuongeza Uelewa wa Upatikanaji, matumizi na Usambazaji wa Taarifa za Hali ya Hewa iliyofanyika katika ukumbi wa FDC, Handeni, Tarehe: 19 Disemba 2020.
“Kutafsiri taarifa za hali ya hewa kunahitaji utaalamu, wananchi wengi hawana utaalamu huo, hivyo kupata nafasi ya warsha hii ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa yanafanyika na kuleta mafanikio ya kiuchumi kwa Taifa letu, Dkt. Kabelwa yeye mwenyewe amekuwa akituma taarifa kupitia mitandao ya kijamii ili zitufikie wanahandeni kwa wakati, na taarifa ya msimu wa Vuli mwaka huu imeeleza uwepo wa mvua chache, naendelea kusisitiza tutumie vizuri nafasi hii”. Alizungumza Mhe. Nguvila.
Mhe. Nguvila aliendelea kuzungumza kuwa elimu ya kuongeza uelewa imekuja wakati muafaka kwa kutambua kuwa takribani asilimia 90 ya wananchi wa Handeni ni wakulima, hivyo kupata taarifa sahihi na kwa wakati hususan msimu wa kilimo ni jambo la muhimu sana.
“Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiboresha sana Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuwapatia mitambo ya kisasa ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa umma ni za uhakika na usahihi wa hali ya juu”. Alisisitiza Mhe. Nguvila
Awali, wakati akizungumza kwenye ufunguzi, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa alimshukuru Mgeni Rasmi kwa kufungua warsha hiyo ambayo ni mara ya piliu, ambapo ya kwanza ilifanyika mwaka 2017 na kuwataka washiriki wote kuendeleza ushirikiano wa kuhakikisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa yanaleta tija.
“Warsha hii imejumisha wadau mbalimbali wakiwemo madiwani, watendaji kata, maafisa ugani, walimu, wakulima na RedCross, nawaomba wadau wote kuendelea kuwa mabalozi wa TMA”. Alifafanua Dkt. Kabelwa
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji-Handeni, Bw. Kenneth Haule alifurahishwa na uwepo wa warsha hiyo na kueleza kuwa hali ya hewa ni muhimu sana, hasa ikizingatiwa kilimo ni uti wa mgongo.
Kwa upande wa Katibu Tawala, Handeni, Bw. Mashaka Mgeta alisema, hivi sasa kumekuwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo ni vyema kutekeleza maelekezo ya wataalamu wa hali ya hewa ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo.
Akifunga warsha hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji-Handeni aliwataka madiwani wote kuifanya elimu ya hali ya hewa kuwa ajenda kuu katika utekelezaji wa majukumu yao, na kuishukuru TMA kwa jitahada zake.
Warsha hiyo imeandaliwa na TMA kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Shirika la Kimataifa la Korea (KOICA)
No comments:
Post a Comment