Thursday, November 5, 2020
SIKU YA TSUNAMI DUNIANI 2020
Dar es Salaam, Tarehe 05 Novemba 2020:
Kila ifikapo Tarehe 05 Novemba, Dunia huadhimisha Siku ya Tsunami Duniani, hii ni kutokana na makubaliano ya mwaka 2015 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo ilikubalika kuwa na siku ya kimataifa ya kutoa elimu ya Tsunami. Maadhimisho ya mwaka huu yanaadhimishwa na kauli mbiu “Utayari kwa Wimbi la Tsunami”. Kauli-mbiu hii ni mahususi hasa tukizingatia kumekuwa na ongezeko la matetemeko ya ardhi chini ya bahari ya hindi. Mfano ni tememeko lililotokea hivi karibuni tarehe 12 Agosti, 2020 majira ya saa 2 usiku lenye ukubwa wa kipimo cha ritcha 5.9 katika eneo la kusini mashariki mwa Mkoa wa Pwani katika bahari ya Hindi.
Nini maana ya Tsunami:
Tsunami ni mfululizo wa mawimbi makubwa ya maji yanayofikia urefu wa mita 30 na kusafiri kwa kasi ya kufikia kilomita 950 kwa saa, mawimbi haya yanaweza kutokana na tetemeko la ardhi chini ya bahari, maporomoko ya ardhi, milipuko ya volkano, milipuko ya nyuklia na kuanguka kwa vimondo baharini ambavyo husababisha kuhamisha ghafla kiasi kikubwa cha maji ya bahari yaliyo na nguvu kubwa na kusafiri kwa kasi.
Jina la mawimbi haya yaani Tsunami limetokana na maneno ya Kijapani ‘tsu’ na ‘nami’ ni maana ya ‘bandari’ na ‘wimbi’
Matukio ya Tsunami:
Matukio ya Tsunami kwa kawaida hutokea mara chache, hata hivyo Tsunami hutokea ghafla na madhara yake ni makubwa kuliko aina nyingine za majanga. Mfano ni tukio la Japan lilitokea mwaka 2011, lililosababishwa na tetemeko la ardhi chini lenye ukubwa wa kipimo cha ritcha 9.0 katika Pwani ya bahari ya Pasifiki na baadhi ya matukio mengine kama la 2004 lilitokea maeneo ya Indonesia na mawimbi yake kufika katika pwani ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.
Hivyo, serikali za nchi za ukanda wa bahari ya Hindi kupitia Kamisheni yake ya masuala ya Bahari (Intergovernmental Oceanographic Commission-IOC) inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO zimefanya kazi kubwa kujenga mfumo wa tahadhari ya tsunami unaohusisha upimaji na utoaji wa tahadhari.
Katika eneo hili kwa upande wa Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inashirikiana kikamilifu na Idara ya Uratibu Maafa (Ofisi ya Waziri Mkuu) katika kuhakikisha tahadhari ya tsunami inatolewa ipasavyo na hatua stahiki zinachukuliwa ili kupunguza maafa.
Athari:
Tsunami husababisha upotevu wa maisha ya watu wengi na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu katika muda wa dakika chache tu kutokana na mafuriko katika ukanda wa pwani.
Elimu kwa jamii:
Programu za kujenga uelewa kwa jamii zilizo katika maeneo hatarishi ya Tsunami zimeendelea kutekelezwa ili kuhakikisha jamii inaweza kuchukua hatua stahiki za kujinasua kutoka eneo lenye hatari ya tsunami pindi tahadhari inapotolewa.
Katika kuhakikisha mfumo wa tahadhari unafanya kazi ipasavyo, kila mwaka Tanzania hujihusisha katika maandalizi ya kukabiliana na Tsunami kwa kushiriki katika mazoezi ya kupima uwezo wa miundombinu ya mawasiliano katika nchi za ukanda wa bahari ya Hindi.
Mwezi Septemba, 2018 Tanzania ilishiriki katika zoezi la kukabiliana na janga la Tsunami katika bahari ya Hindi. Zoezi hilo lilishirikisha wadau wa nchi 24 zinazozunguka Bahari ya Hindi. Zoezi hili hufanyika kila baada ya miaka miwili, hivyo kwa mwaka huu wa 2020 hapa nchini lilifanyika tarehe 20 Oktoba na kuhusisha wadau kutoka taasisi na Mamlaka ya Mkoa wa Dar es salaam. Katika zoezi la mwaka huu, Jukwaa la uratibu Maafa la Mkoa wa Dar es salaam (DarMAERT) lilitumika katika kupima utayari wa mifumo ya mawasiliano na miongozo ya kiutendaji katika kukabiliana na tsunami kwa wilaya za Ilala na Kinondoni.
Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Featured Post
DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.
Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...
-
10 Septemba 2024, Arusha: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa elimu kwa wadau mbalilmbali wa Ununuzi kuhusu matumizi sahihi ya h...
-
06 Septemba 2024, Dar es Salaam: Wahandisi nchini wamekumbushwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa sambamba na kuchangia gharama za upatik...
-
DODOMA; Tarehe 19 Agosti, 2024; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na...
No comments:
Post a Comment