Wanahabari katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza. |
Wadau katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza. |
Mmoja wa wadau akichangia mada wakati wa warsha ya wanahabari ya kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari zinazoweza kujitokeza. |
Tarehe
09/10/2019: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana
na wadau wa sekta mbalimbali na wanahabari ili kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua
za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 na athari
zinazoweza kujitokeza.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, mgeni
rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt.
Agnes Kijazi alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kusambaza taarifa
za hali ya hewa ukiwemo utabiri wa hali ya hewa na tahadhari ya hali mbaya ya
hewa, huku akitolea mfano wa athari zilizoanza kuonekana mwanzoni mwa msimu wa
mvua za vuli za mwaka huu.
“Napenda kusisitiza umuhimu wa warsha hizi ni
kuhakikisha jamii tunayoenda kuihudumia inapata taarifa sahihi, kwa wakati na
kwa lugha inayoeleweka kirahisi, msimu wa vuli umeanza na matukio mengi ya
upepo mkali, mawimbi makubwa na mvua kubwa hivyo taarifa hizi zinakuwa na
manufaa pale ambapo zinatumika kwa wakati’, alisema Dkt. Kijazi. Aidha,
alivishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kusambaza kwa wakati
taarifa za hali ya hewa ikiwa pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa.
Kwa upande mwingine, Dkt.Kijazi alifafanua kwa
wadau wa sekta mbalimbali sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya 2019.
Alisema lengo la Sheria hiyo ni kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini na
kutoa mwongozo wa ushiriki wa sekta mbalimbali
katika matumizi ya huduma hizo. Dkt. Kijazi alifafanua vipengele vya
sheria hiyo vinavyowahusu wadau wa huduma za hali ya hewa alipokuwa anafunga
mkutano huo wa wadau.
Aidha, wadau hao walipata fursa ya kutoa ushauri wa
athari zinazoweza kujitokeza kulingana na utabiri wa msimu wa mwaka ulioandaliwa
kwa mikoa inayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ambayo ni mikoa ya kanda ya magharibi, kati,
nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini
pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wa wanahabari waliahidi kuendelea kutoa
taarifa sahihi za hali ya hewa kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania na waliishukuru TMA kwa kuendesha warsha hizo ambazo zimeendelea
kuwajengea uwezo wa kuelewa lugha inayotumika katika utabiri wa hali ya hewa.
Warsha hizo
zilifanyika tarehe 08/10/2019 kwa kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali na
tarehe 09/10/2019 kwa kuwakutanisha wanahabari. Utabiri wa msimu wa mvua za mwaka
kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 unatarajiwa kutolewa rasmi kwa
umma kupitia vyombo vya habari siku ya Alhamisi, tarehe 10/10/2019,makao makuu
ya ofisi za TMA, saa tano kamili asubuhi.
No comments:
Post a Comment