Dar es Salaam,Tarehe 10/10/2019: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri
wa msimu wa mvua za mwaka (Novemba 2019 hadi Aprili 2020) na athari zinazoweza
kujitokeza. Utabiri huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara moja
kwa mwaka ikiwa ni mikoa ya Kigoma, Tabora,Rukwa,Katavi,Mbeya, Songwe,
Njombe,Iringa, Lindi, Dodoma, Singida, Mtwara na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na waandishi
wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa WMO Dkt. Agnes
Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo kwa kupata
ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika kwa vile maeneo mengi yanatarajiwa
kuwa na mvua za kutosha.
‘Naendelea kutoa rai kwa
wananchi wa mikoa husika kuzitumia mvua hizi kwa kupanda mazao sahihi kwa
kufuata ushauri wa wataalamu, kama tunavyoona maeneo mengi yatarajiwa kuwa na
mvua za juu ya wastani hadi wastani’, alisema Dkt. Kijazi.
Aidha, Dkt. Kijazi
alifafanua kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi
kwa kusema kuwa mvua hizi ni za msimu wa vuli kwa maeneo yanayopata mvua mbili
kwa mwaka na katika kipindi hiki cha vuli kunatarajiwa kuwa na vipindi vifupi
vya mvua kubwa ambapo alimalizia kwa kuwataka wananchi kuendelea kufuatilia
taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA sambamba na kuchukua tahadhari ya
vipindi vifupi vya mvua kubwa,upepo mkali na mawimbi makubwa, vinavyotarajiwa
kujitokeza katika baadhi ya maeneo.
Utabiri uliotolewa kwa
maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka unaonesha maeneo ya mengi
ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Rukwa
Kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara, yanatarajiwa kupata mvua za juu
ya wastani hadi wastani na maeneo ya mikoa ya Kigoma na Katavi, yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu
ya wastani.
No comments:
Post a Comment