Wadau wa Maendeleo katika picha ya pamoja na mgeni rasmi wakati wa uzinduzi rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoka kuwa Wakala (Agency) katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam |
Tarehe 05/09/2019: Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwele amezindua rasmi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoka kuwa Wakala (Agency) katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Uzinduzi wa Mamlaka umetokana na sheria ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa “Tanzania Meteorological Authority Act No.2 of 2019”
iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusainiwa tarehe
13 Februari, 2019 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, awali Wakala huo ulianzishwa baada ya iliyokuwa Idara Kuu ya Hali
ya Hewa kubadilishwa na kuwa Wakala wa Serikali mnamo mwaka 1999 kwa Sheria yaw
akala wa Serikali sura 245 marejeo ya 2002.
Idara Kuu ya Hali ya
Hewa (Directorate of Meteorology) ambayo ilianzishwa mwaka 1977 baada ya
kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ilikuwa na jukumu la kuangaza na
kutoa taarifa za hali ya hewa nchini. Kabla ya hapo huduma hizo zilikuwa
zikitolewa na Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Mashariki (EAMD).
Akizungumza wakati wa uzinduzi
huo, Mhe. Kamwelwe aliwajulisha washiriki kwamba ndege yetu iliyokuwa
inashikiliwa Afrika Kusini imekwishawasili nchini baada ya Serikali kushinda
kesi. Mheshimiwa Kamwelwe alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi
kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani.
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa
Bodi ya Ushauri ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi kwa usimamizi mzuri wa Mamlaka. Akizungumzia
uzinduzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Mheshimiwa Kamwelwe alisema Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania ‘Tanzania
Meteorological Agency’ imepandishwa hadhi na kuwa Mamlaka, hivyo kuweza kukidhi
pande zote mbili za Tanzania Bara na Visiwani
Wakati akitoa neno la ukaribisho,
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Chamuriho alisema huduma za hali ya
hewa ni mtambuka zinahitajika katika sekta zote ikiwemo ya viwanda, kwa hiyo
wageni wote waalikwa wako katika uzinduzi huo kutokana na umuhimu wa huduma
hizo za hali ya hewa
Aidha, wakati akiwasilisha
taarifa ya uzinduzi TMA na mifumo mbalimbali ya kiutendaji, Mkurugenzi Mkuu wa
TMA Dkt. Agnes Kijazi alielezea kuwa Mamlaka
imeongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu utoaji na utumiaji wa huduma za
hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na alikabidhi hati kutoka
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) za kutambua rasmi vituo vya Songea na
Bukoba kuwa na takwimu za muda mrefu za zaidi ya miaka 100.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Ndugu. Mustafa A. Jumbe aliwasisitiza kuwa hali ya hewa haina mipaka na
kudhihirisha jinsi Tanzania Visiwani wanavyozingatia tahadhari zinazotolewa na
TMA kwa usafiri wa baharini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alielezea mafanikio ya uongozi wa Bodi
anayoiongoza ikiwa ni kupatikana kwa sheria iliyopelekea kuzindua Mamlaka hiyo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa
na viongozi mbalimbali wa serikali, wakurugenzi wa taasisi, wawakilishi wa
sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya kimaendeleo, wanahabari na
wafanyakazi wa TMA. Ulienda sambamba na uzinduzi wa nembo mpya, tovuti
mpya na mifumo ya “TMA Digital Meteorological Observatory (TMA-DMO)” kwa ajili
ya kurahisisha mawasiliano ya Data za Hali ya Hewa; “Meteorological Aviation
Information System (MAIS)” kwaajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za hali ya
hewa katika usafiri wa anga na “ Marine Meteorological Information System
(MMIS)” unaosaidia sana katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya kwenye
maji yaani bahari, maziwa na mito
No comments:
Post a Comment