Na: Monica Mutoni. Geneva
13/06/2019
Kwa
mara nyingine Tanzania imeingia katika historia ya kimataifa kwa
Mkurugennzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na mwakilishi wa
kudumu Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuibuka
mshindi wa nafasi ya umakamu wa tatu wa Rais wa WMO. Dkt. Kijazi
anachukua nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2019-2022
akiwa mwanamke wa kwanza na mjumbe wa kwanza kutoka nchi zinazoendelea
kushika nafasi hiyo. Dkt. Kijazi atakuwa na majukumu makubwa ya
kumsaidia Rais kuongoza shirika hilo katika kutekeleza majukumu yenye
tija kwa wanachama wake ikiwemo Tanzania
Akizungumzia
ushindi wake mbele ya wapiga kura wa mkutano wa 18 wa Shirika la Hali
ya Hewa Duniani (WMO) na wajumbe waalikwa, Dkt. Kijazi alitoa shukrani
zake za dhati kwa wote waliomwamini na kumuunga mkono hadi kufika kupata
nafasi hiyo na kuahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa weledi wa hali ya juu
ili kufikia malengo ya shirika hilo.
‘ Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote waliokuwa pamoja na mimi kwa
kuniunga mkono na kunichagua kwa kura zote, naahidi kuitumikia nafasi
hii kwa weledi mkubwa na kuhakikisha WMO inafikia malengo yake’. Alisema
Dkt Kijazi
Akizungumzia ushindi huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Atashasta Nditiye alisema ni heshima kubwa sana kwa nchi, Wizara inampongeza sana Dkt. Kijazi na kuamini kuwa ataiwakilisha nchi vizuri, aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano aliouonesha kwa kukubali Tanzania kuwakilishwa na Dkt. Kijazi ambapo kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya hali ya hewa kumeendelea kuiletea sifa nchi kwa ujumla
Kwa upande wa
Kaimu Balozi, Ubalozi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Geneva Ndugu. Robert
Kahendaguza alisema kuwa ushindi wa Dkt. Kijazi ni kielelezo cha
umadhubuti wa kidiplomasia ya Tanzania na sifa zake binafsi ikiwemo
uzoefu wa muda mrefu na elimu ya ngazi ya juu katika nyanja ya sayansi
ya hali ya hewa, aidha aliongeza kuwa sababu za sifa hizo ziliupunguzia
ubalozi kazi ya kumnadi na hata kuwa rahisi kuishawishi nchi ya Sudan
kuondoa mgombea wao na hivyo kumfanya Dkt. Kijazi kuwa mgombea pekee
katika uchaguzi huo.
Uchaguzi
wa viongozi wa WMO hufanyika kila baada ya miaka minne kwa kuchagua
viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais wa
kwanza, wa pili na wa tatu, ambapo kwa mwaka huu umefanyika katika mkutano
wa 18 wa shirika hilo baada ya muda wa viongozi hao kuisha. Uchaguzi
huo ulifanyika kwa haki na kwa amani na kuwapata viongozi hao ambao ni
Prof. Petteri Taalas kutoka Finland (Katibu Mkuu), Prof. Dk. Gerhard
Adrian kutoka Ujerumani (Rais), Prof. Celeste Saulo kutoka Argentina
(Makamu wa kwanza wa Rais), Dr. Albert Martis kutoka Curacao (Makamu wa
Pili wa Rais) na Dkt. Agnes Kijazi kutoka Tanzania (makamu wa tatu wa
Rais).
No comments:
Post a Comment