Bodi ya
Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imempongeza Dkt. Agnes Kijazi,
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na katibu wa hiyo kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa
makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Akizungumzia
pongezi hizo na ushindi uliopatikana wakati wa kikao cha 55 cha Bodi,
mwenyekiti wa Bodi Dkt. Buruhani Nyenzi aliwasilisha pongezi za dhati kutoka
kwa wajumbe wote na kukiri kuwa nafasi iliyopatikana ni moja ya njia za kuzidi
kuipandisha Tanzania juu katika anga za kimataifa.
‘Bodi inatoa
pongezi za dhati kwa Dkt. Kijazi kwa kuchaguliwa kushika nafasi ya juu WMO, kwa
kuwa kupitia nafasi hiyo Tanzania inazidi kupanda juu katika anga za
kimataifa’. Aliongea Dkt. Nyenzi
Mwenyekiti
huyo aliendelea kuwakumbusha washiriki wa kikao hicho kuwa mafanikio ambayo
Tanzania imeyapata yanachangiwa na mambo mengi. Alisema jambo la kwanza na la
muhimu ni sifa za Dkt. Kijazi kama mgombea wa nafasi hiyo, pili kukubalika na
kukua kwa diplomasia ya Tanzania nje ya nchi na tatu sifa nzuri za Watanzania
ambao wamewahi kufanya kazi WMO akiwemo yeye mwenyewe.
Aidha, Dkt.
Nyenzi alionesha furaha yake namna ambavyo TMA inafanya kazi kwa umoja na
upendo baina ya wafanyakazi, akitolea mfano mapokezi yaliyofanywa na
wafanyakazi kwa kiongozi wao ambaye ni Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi
alichaguliwa kuwa makamu wa tatu wa Rais wa WMO kwenye mkutano wa 18 wa shirika
hilo uliofanyika jijini Geneva, Uswisi tarehe 03-14 Juni 2019 kwa kipindi cha
miaka minne, akiwa mwanamke na makamu wa tatu wa Rais wa kwanza kutoka nchi
zinazoendelea hususani nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
IMEANDALIWA NA;
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)
No comments:
Post a Comment