Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendesha
warsha maalum kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kisiwani Pemba kuhusu huduma za hali ya hewa katika bahari ya
Hindi ili kuboresha uelewa wa matumizi sahihi ya taarifa zitolewazo na TMA.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, mgeni rasmi Mhe. Hemed
Suleiman Abdala ambaye pia ni mkuu wa mkoa Pemba Kusini aliwataka washiriki
kutambua lengo la semina ni pamoja na kupata uelewa wa matumizi sahihi ya
utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za kila siku zinazotolewa na TMA ili kukidhi malengo ya huduma hizo nchini.
Katika hotuba yake mgeni rasmi alisisitiza kwa kutambua mchango mkubwa
toka TMA katika kuboresha uelewa wa wadau toka katika sekta mbalimbali hapa
nchini juu ya matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa
na kufurahishwa na hatua ya kufika kisiwani Pemba.
“Napenda kuishukuru na kuipongeza
TMA kwa kuandaa na kufanikisha warsha hii muhimu kufanyika kisiwani Pemba
kwani itasaidia kutuepusha na maafa hususani
wavuvi, hasa wale wachache wanaofanya shughuli zao kwa mazoea na kupelekea
kukumbwa na maafa” alisema mkuu wa mkoa wa Pemba.
Aidha alimalizia kwa kuwataka washiriki wawe mabalozi wazuri katika
maeneo yao ya kazi kwa kutoa elimu hiyo muhimu ambayo itasaidia kujiepusha na
maafa yanayoweza kujitokeza.
IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
No comments:
Post a Comment